SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limekutana na wadau wa sekta ya petroli na bidha zake kujadili viwango vya petroli vilivyoboreshwa kwa lengo la kuimarisha ubora wa mafuta, kulinda afya za wananchi na kuhifadhi mazingira

Akizungumza katika mkutano wa wadau uliofanyika leo, Oktoba 27, 2026, Kaimu Mkurugenzi wa Uandaaji Viwango TBS, Nickonia Mwambene amesema mkutano huo unalenga kuwawezesha wadau kuelewa viwango hivyo, ikiwemo mabadiliko ya baadhi ya vigezo na taratibu za utekelezaji wake.

Amesema viwango hivyo vimeandaliwa katika ngazi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kwa kushirikisha Tanzania, na kuchapishwa baada ya kupitia taratibu zinazohusisha mashauriano ya wadau na maoni ya umma kabla ya kupitishwa kuwa viwango vya kitaifa.

Ameeleza kuwa mabadiliko ya teknolojia katika sekta ya nishati duniani na kikanda yameifanya mifumo ya viwango kuhusisha si tu ufanisi katika utendaji wa mafuta, bali pia masuala ya afya, uendelevu wa mazingira na ulinganifu wa masharti ya biashara ya kimataifa.

Amesema, majadiliano hayo pia yanalenga kuweka mwongozo wa utekelezaji na kipindi cha mpito katika sekta ya mafuta, kwa kuzingatia sheria na kanuni zinazotumika, huku yakihakikisha kuwa mahitaji ya kitaifa yanaendana na mifumo ya kikanda bila kusababisha usumbufu katika soko au upatikanaji wa mafuta.

Amesema ushirikiano wa wadau ni muhimu katika kuhakikisha soko linapata mafuta yenye ubora unaotakiwa, huku mazingira yakilindwa na sekta ya nishati ikiendelea kuchangia maendeleo ya uchumi wa nchi.