​Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es salaam

MAMLAKA ya Udhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) kupitia Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NEST) umewezesha utoaji wa zabuni za tenda 403,643 zenye thamani ya Shilingi trilioni 42.6, kufanikiwa kuokoa takribani Shilingi bilioni 28 kutokana na kupunguza matumizi ya karatasi na nyaraka mbalimbali za ununuzi.

​Akizungumza leo, Oktoba 29, 2026, jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Bw. Dennis Simba, wakati wa kikao kazi kati ya mamlaka hiyo, wahariri, na waandishi wa habari kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR)amesema kiwango Cha uzingatiaji wa sheria za Ununuzi wa Umma kuongezeka kutoka asilimia 65 mwaka wa fedha 2023/24 hadi asilimia 79 mwaka 2025/26 hii ni baadhi ya makampuni kufungiwa kushindwa kutii sheri.

Mkurgenzi PPRA amesema Mfumo wa Ununuzi wa Umma kwa njia ya Kielektroniki (NeST) umewezesha kutolewa kwa zabuni 430,643 zenye thamani ya Sh trilioni 42.6 tangu kuanza kutumika kwake Septemba 2023.

Amesema mfumo huo ulioanzishwa na Serikali kwa lengo la kuboresha usimamizi wa ununuzi wa umma, umeelezwa kusaidia kuongeza uwazi, ushindani, uwajibikaji na ufanisi katika matumizi ya fedha za umma, huku ukiwapa wazabuni fursa ya kushiriki zabuni bila kulazimika kufika kwenye taasisi nunuzi.

Kwa mujibu wa taarifa ya PPRA, matumizi ya mfumo huo yamechangia kuongezeka kwa kiwango cha uzingatiaji wa sheria za ununuzi wa umma kutoka asilimia 65 mwaka wa fedha 2023/24 hadi asilimia 76 mwaka 2024/25 na kufikia asilimia 79 mwaka 2025/26.

PPRA imeeleza kuwa mfumo huo pia umewezesha kuokoa gharama zinazotokana na matumizi ya karatasi, baada ya kuzuia uchapishaji wa zaidi ya kurasa milioni 288.57 za nyaraka za zabuni, hatua inayokadiriwa kuokoa Sh bilioni 27.64.

Aidha, matumizi ya NeST yamechangia kupunguza muda na gharama za wazabuni kushiriki zabuni za Serikali kwa kuwa michakato hiyo sasa inafanyika kwa njia ya kielektroniki.

“Utafiti uliofanyika umeonesha mfumo huo kuchangia kupungua kwa uzalishaji wa gesi chafuzi kwa tani 64,768 za hewa ya ukaa kwa mwaka katika kipindi cha 2023/24 hadi 2024/25” amesema.

Katika hatua nyingine, PPRA inaendelea na utafiti unaolenga kuwezesha mfumo huo kusajiliwa katika biashara ya kaboni, ambapo inatarajiwa kuchangia mapato yanayozidi Sh bilioni 20 kwa mwaka kupitia mauzo ya kaboni.

Katika kuhakikisha fursa za ununuzi wa umma zinawafikia wananchi wengi zaidi, PPRA imeeleza kuwa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023 na Kanuni zake za mwaka 2024 zimeweka masharti ya upendeleo kwa wazabuni wa ndani na makundi maalumu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, zabuni zenye thamani isiyozidi Sh bilioni 50 zimetengwa kwa wazabuni wazawa, huku wazabuni wa ndani wakipewa upendeleo wa hadi asilimia 10 katika zabuni zinazohusisha ushindani wa kimataifa. Pia, bidhaa zinazozalishwa nchini zimewekewa upendeleo wa hadi asilimia 15 dhidi ya bidhaa kutoka nje.

Kwa upande wa makundi maalumu, taasisi za umma zinatakiwa kutenga asilimia 30 ya bajeti zao za ununuzi kwa ajili ya vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.

PPRA imesema hadi sasa makundi maalumu 33,659 yamesajiliwa kwenye mfumo huo, yakiwemo makundi ya vijana 16,133, wanawake 16,070, wazee 767 na watu wenye ulemavu 689.

Makundi hayo yamepata zabuni zenye jumla ya thamani ya Sh bilioni 82.34, ambapo vijana wamepata zabuni za Sh bilioni 44.74, wanawake Sh bilioni 33.15, wazee Sh bilioni 3.78 na watu wenye ulemavu Sh milioni 680.21.

Ameongeza kuwa PPRA imeweka lengo la kuongeza idadi ya makundi maalumu yaliyo tayari kushiriki zabuni hadi kufikia 300,000, kwa kuzingatia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

“Katika kutekeleza lengo hilo, wananchi wanahamasishwa kuunda vikundi vya watu watatu au zaidi, kuvisajili katika halmashauri zao na baadaye kujisajili kwenye mfumo wa NeST ili kupata fursa za zabuni za Serikali.

“Mfumo huo umeendelea kuboreshwa kwa kuunganishwa na mifumo mingine zaidi ya 30, ikiwemo ya benki, malipo, leseni na usajili wa wataalamu, hatua inayosaidia kurahisisha uhakiki wa nyaraka na kupunguza uwezekano wa matumizi ya nyaraka za kughushi.

“Aidha, mfumo huo umeunganishwa na Benki ya NMB kwa ajili ya uhakiki wa dhamana za zabuni, huku benki za TCB na CRDB zikiwa katika hatua za mwisho za kuunganishwa. Kupitia Bank Security Portal iliyoanza kutumika Oktoba 1, 2026, zaidi ya benki 36 zimeunganishwa ili kuwezesha utoaji na uhakiki wa dhamana za zabuni kwa njia ya kielektroniki” amesema.

Kwa upande wa matumizi ya teknolojia ya simu, PPRA imeanzisha programu ya NeST Tenderer inayopatikana kwenye Play Store na App Store, ambayo inawawezesha watumiaji kujisajili, kuomba zabuni na kufuatilia malipo yao kupitia simu janja.

Mfumo huo pia umeendelea kupata utambuzi wa kimataifa. Mwaka 2024, ulipata tuzo ya Mfumo Bora Zaidi wa Ununuzi wa Umma Barani Afrika katika tuzo za African Association for Public Administration and Management (AAPAM) zilizofanyika Kampala, Uganda.

Mwaka 2026, NeST ulitambuliwa miongoni mwa mifumo 20 bora ya Serikali Mtandao duniani katika tuzo za World Summit on the Information Society (WSIS) zilizofanyika Geneva, Uswisi, Julai 8. Pia, Septemba 21, 2026, ulitajwa miongoni mwa mifumo 15 bora ya Serikali ya Kidijitali duniani katika tuzo za Digital@UNGA2026 zilizofanyika New York, Marekani.

Katika kuimarisha uelewa wa wadau, PPRA imeendelea kutoa mafunzo kwa watumishi wa taasisi nunuzi, wazabuni, makundi maalumu, wanafunzi, wabunge na waandishi wa habari. Katika kipindi cha Julai 2023 hadi Septemba 2026, zaidi ya watumishi 200,000 wa taasisi nunuzi, wazabuni zaidi ya 20,000 na wanafunzi zaidi ya 500,000 wa vyuo vya elimu ya juu wamefikiwa kupitia mafunzo hayo.

PPRA pia imeendelea kutoa elimu kwa umma kupitia redio, televisheni, mitandao ya kijamii na filamu ya elimu iitwayo Winga, kwa lengo la kuwahamasisha wananchi kutumia fursa za zabuni za Serikali.

Mamlaka hiyo imewataka Watanzania kuchangamkia fursa za ununuzi wa umma kwa kujiunga na vikundi, kujisajili kwenye NeST na kushiriki katika michakato ya zabuni kwa kuzingatia sheria, uwazi na uadilifu.

Kwa mujibu wa PPRA, matumizi ya mfumo huo ni sehemu ya jitihada za kujenga uchumi jumuishi unaowezesha wananchi wengi zaidi kushiriki katika shughuli za kiuchumi na kuchangia maendeleo ya Taifa.

.