Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Zanzibar inalenga kuimarisha ushirikiano wa moja kwa moja na Kisiwa cha Jeju katika utalii endelevu, uchumi wa buluu, nishati mbadala, biashara na uwekezaji, pamoja na elimu na mafunzo, ili Zanzibar na Jeju zinufaike na uzoefu na fursa zilizopo.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 29 Oktoba 2026, alipokutana na Gavana wa Jeju, Mhe. Wi Seong-gon, Jeju, Jamhuri ya Korea (Korea Kusini).
Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt. Mwinyi amependekeza kuanzishwa kwa ushirikiano wa kindugu kati ya Zanzibar na Jeju, utakaojenga msingi wa ushirikiano wa muda mrefu na kuweka maeneo ya kipaumbele pamoja na utaratibu wa utekelezaji wake.
Amesema katika utalii, Zanzibar inaweza kunufaika na uzoefu wa Jeju katika usimamizi wa maeneo ya utalii, utalii wa mazingira, mafunzo ya huduma z
kwa wageni na uhifadhi wa urithi wa utamaduni.
Aidha, ushirikiano huo unaweza kujikita katika uvuvi endelevu, ufugaji wa samaki, uhifadhi wa rasilimali za bahari na kuongeza thamani ya bidhaa za baharini.
Dkt. Mwinyi ameeleza umuhimu wa kushirikiana katika nishati mbadala na mazingira, ikiwemo nishati safi, usimamizi wa taka na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Amesema Jeju ina uzoefu mkubwa katika matumizi ya nishati ya jua na upepo, ambayo kwa pamoja inachangia takribani asilimia 30 ya umeme unaotumika kisiwani humo.
Katika biashara na uwekezaji, Rais Dkt. Mwinyi amewakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara wa Jeju kuangalia fursa zilizopo Zanzibar katika miundombinu ya utalii, uvuvi, ufugaji wa samaki, usarifu wa mwani na nishati mbadala, sambamba na ushirikiano wa teknolojia.
Naye, Gavana wa Jeju, Mhe. Wi Seong-gon, ameeleza utayari wa kuendeleza ushirikiano na Zanzibar, huku akikubaliana kuanza majadiliano ya kitaalamu na kuweka utaratibu wa kufuatilia hatua zinazofuata.












