• Kesi ya tatu ya uhaini yafikia hukumu Ijumaa hii jijini Dar es Salaam
• Tangu Bibi Titi, Lifa Chipaka na wenzao, kisha Uncle Tom, Hatty MacGhee na wenzao, sasa ni Lissu peke yake
Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Macho na masikio ya Watanzania yanaelekezwa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, ambako Ijumaa, Novemba 6, 2026, hukumu ya kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, inatarajiwa kutolewa.
Ni wiki ya uamuzi kwa mwanasiasa huyo, baada ya safari ndefu ya kisheria iliyoanza Aprili 9, 2025, alipokamatwa Mbinga, mkoani Ruvuma, muda mfupi baada ya kuhutubia mkutano wa hadhara.
Hukumu inatarajiwa kutolewa na jopo la majaji watatu, likiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, akisaidiwa na majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.
Kwa kumbukumbu za kesi kubwa za uhaini Tanzania Bara, shauri la Lissu linafuata yale yaliyowakabili Bibi Titi Mohamed na wenzake mwaka 1970, pamoja na Pius Lugangila (Uncle Tom), Hatibu Gandhi, maarufu Kapteni Hatty MacGhee, na wenzao mwaka 1983.
Hivyo, takribani miaka 40 tangu Mahakama ya Rufani ilipohitimisha kesi ya MacGhee na wenzake Desemba 14, 1987, Mahakama Kuu inajiandaa kutoa uamuzi katika shauri jingine la uhaini lililovuta hisia za wananchi.
Uncle Tom aliondolewa kwenye orodha ya washitakiwa baada ya kutoroka gerezani Ukonga jijini Dar es Salaam na kukimbilia Kenya, kisha Uingereza.
Tofauti na kesi mbili zilizotangulia, zilizohusisha washtakiwa wengi, Lissu anakabiliwa na shtaka hilo akiwa peke yake.
Shtaka lake, chini ya Kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linatokana na kauli anazodaiwa kutoa Aprili 3, 2025, katika kampeni ya CHADEMA ya No Reforms, No Election.
Upande wa mashtaka unadai kuwa kauli hizo zililenga kuhamasisha wananchi kuzuia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 na kuitisha Serikali.
Lissu amekanusha shtaka hilo, akisisitiza kuwa kauli zake zilihusu madai ya mageuzi ya mfumo wa uchaguzi na hazikufikia kiwango cha kosa la uhaini.
Aprili 10, 2025, siku moja baada ya kukamatwa, Lissu alifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, na kusomewa shtaka la uhaini pamoja na mashtaka mengine yaliyohusiana na uchapishaji wa taarifa za uongo.
KWA HABARI ZAIDI SOMA GAZETI LA JAMHURI LA NOVEMBA 3-9, 2026



