Na Heri Shaaban, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mkoa wa Dar es Salaam unatarajia kuzindua kampeni maalumu ya usafi wa mazingira, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuimarisha usafi na kukabiliana na uchafuzi wa mazingira katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Dar es Salaam Novemba 6, 2026 , Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila, amesema uzinduzi wa kampeni hiyo utafanyika Novemba 14, 2026 katika viwanja vya Posta Kijitonyama kuanzia asubuhi, huku ukiwa na kaulimbiu isemayo “Dar es Salaam Safi Inawezekana, Tushirikiane Pamoja.”
Akizungumza kuhusu maandalizi ya kampeni hiyo, Chalamila amesema hatua hiyo inatokana na msisitizo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, kuhusu umuhimu wa usafi na utunzaji wa mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Chalamila amesema kuwa uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam umejipanga kuhakikisha kampeni hiyo inatekelezwa kwa ushirikiano wa wakuu wa wilaya, madiwani, wabunge, wakurugenzi na wadau mbalimbali wa usafi.
Amesema siku ya uzinduzi kutakuwa na shughuli mbalimbali, ikiwemo kushiriki zoezi la usafi pamoja na wadau na kugawa vifaa vya usafi kama vile mapipa ya taka (dustbins) kwa ajili ya kuimarisha usafi katika maeneo ya umma.
Aidha, amewapongeza wadau waliojitokeza kuchangia vifaa hivyo, akiwataja kampuni ya Standard na GNM Cargo kuwa miongoni mwa walioonyesha ushirikiano katika kufanikisha kampeni hiyo.
Chalamila ametoa wito kwa kampuni, taasisi na wadau wengine kujitokeza kuchangia vifaa na rasilimali zitakazosaidia kufanikisha kampeni hiyo kabla ya uzinduzi wa Novemba 14, 2026.
Amesisitiza kuwa mafanikio ya Dar es Salaam kuwa safi yanahitaji ushiriki wa kila mwananchi, si Serikali pekee, hivyo kila mmoja ana wajibu wa kutunza mazingira na kuzingatia usafi katika maeneo anayoishi na kufanyia shughuli zake.





