Serikali imesema inaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia unaolenga kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kumtua mama kuni kichwani na kupunguza athari za matumizi ya nishati isiyosafi .

Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Mary Francis Masanja, Naibu Waziri wa Nishati alisema Serikali, kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), inaendelea kutekeleza mradi wa kusambaza mitungi ya gesi oevu (LPG) ya kilo sita yenye ruzuku pamoja na majiko banifu yenye ruzuku katika vijiji na vijiji-miji.

Mhe. Salome alisema hatua hiyo inalenga kuongeza upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwa wananchi, hususan wanaoishi vijijini, ambako matumizi ya kuni na mkaa yanaendelea kuwa changamoto kwa kaya nyingi.

Aidha, Serikali inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kutekeleza miradi ya nishati safi ya kupikia katika maeneo ya vijijini, pamoja na kutoa elimu na kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kutumia nishati hiyo.

Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Salome ,ameeleza kuwa elimu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia hutolewa kupitia mikutano, semina na shughuli nyingine zinazolenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Hatua hizo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ajenda ya kitaifa ya kumtua mama kuni kichwani, inayolenga kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, kuimarisha afya za wananchi na kupunguza athari za kimazingira zinazotokana na matumizi ya nishati isiyosafi ya kipikia.

Hata hivyo, katika majibu yake, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome ameeleza lengo la Serikali kuwafikia wananchi wote wa vijijini kutumia nishati safi ya kupikia na zimenufaika na mitungi ya gesi na majiko banifu yenye ruzuku.

Serikali inalenga kufikia asilimia 80 ya Watanzania wanaotumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034, huku utekelezaji wenye matokeo yanayopimika ukiwa muhimu katika kuhakikisha wananchi wa vijijini wananufaika na ajenda hiyo.