Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Arusha

Upatikanaji wa haki katika Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) unakabiliwa na vikwazo vinavyowafanya baadhi ya wananchi kusubiri kwa miaka kusikilizwa; imeelezwa jijini hapa wiki iliyopita.

Hali hiyo inadaiwa kusababisha wengine kufariki dunia kabla ya maombi yao, hata yale ya dharura, kuamuliwa; huku uhaba wa fedha na watumishi, mrundikano wa mashauri na changamoto za utekelezaji wa hukumu vikiibuka kuwa miongoni mwa masuala mazito yaliyoibuliwa wakati wa maadhimisho ya miaka 25 ya mahakama hiyo.

Viongozi wa mahakama na wanasheria wamezitaka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kutoa rasilimali na kutimiza wajibu wa kuheshimu uamuzi, wakionya kuhusu athari za kuendesha taasisi ambayo wananchi wanaifikia lakini wanachelewa kupata msaada wanaoutafuta.

Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Mawakili wa Afrika (PALU), Dan Deya, ameweka mbele ya washiriki hali inayowakabili baadhi ya watu wanaoomba ulinzi wa haraka wa mahakama.

“Unaweza kuandika maombi ya dharura ya amri za muda ili kuokoa maisha, lakini kwa sababu ya mrundikano wa kesi, inachukua miaka miwili kusikilizwa. Tuna watu waliokufa na wateja waliokufa wakati maombi ya dharura na cheti cha dharura yanachukua miaka miwili kupata amri ya muda,” amesema.

Deya hakuweka wazi majina ya waliofariki dunia au namba za maombi husika. Kauli yake, hata hivyo, imeibua uzito wa madhara ya kuchelewa kwa mashauri ambayo waombaji wanayawasilisha wakihitaji hatua za haraka.

“Kama inachukua miaka mitano tangu uandikishe kesi hadi kusikilizwa, hauwezi tena kuzungumzia haki,” amesema.

KWA HABARI ZAIDI ZA KINA SOMA JAMHURI LA NOVEMBA 17 -23, 2026