Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC), David Kafulila, amefafanua umuhimu wa kuwekeza katika rasilimali watu ili kukabiliana na ongezeko kubwa la idadi ya watu nchini, akieleza kuwa kasi hiyo inaweza kuwa baraka au mzigo kwa Taifa.

Akizungumza katika kikao cha kupima mwitikio wa sekta binafsi kuhusu miradi ya ubia (PPP), Kafulila amesema idadi ya Watanzania imeongezeka kutoka 44.9 milioni mwaka 2012 hadi zaidi ya milioni 61 mwaka 2022, na inatarajiwa kufikia milioni 123.4 ifikapo mwaka 2044. Takribani asilimia 42.8 ya wananchi wana umri chini ya miaka 15.

Amesema ongezeko hilo ni fursa ya kiuchumi endapo Serikali itawekeza ipasavyo katika elimu, afya, maarifa na ujuzi. Hata hivyo, Tanzania bado inatumia asilimia 3.3 ya GDP kwenye elimu na asilimia 1.2 kwenye afya, chini ya wastani wa nchi zenye kipato cha chini cha kati.

Kafulila amesisitiza umuhimu wa kutumia ubia na sekta binafsi (PPP) katika kujenga na kuendesha miundombinu ya kibiashara kama masoko, majengo na maegesho, ili Serikali ipate nafasi kubwa zaidi ya kuelekeza rasilimali zake katika huduma za msingi, hususan elimu na afya kwa wananchi wenye kipato cha chini.