Na Pendo Nguka, JamhuriMedia, Dar es Salaam

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Paul Makonda amesema mafanikio ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 yanayotarajiwa kufanyika kwa ushirikiano wa Tanzania, Kenya na Uganda, hayapaswi kupimwa kwa mafanikio ya michezo pekee, bali pia kwa namna yatakavyochochea ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi wa nchi hizo.

Makonda ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi rasmi wa Makao Makuu ya Sekretarieti ya Uratibu wa AFCON 2027 hafla iliyoambatana na makabidhiano ya ofisi kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) pamoja na utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano kati ya CAF na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB).

Amesema ujio wa mashindano hayo makubwa barani Afrika unapaswa kuwa fursa kwa wananchi kunufaika kiuchumi kupitia shughuli mbalimbali zitakazochochewa na uwepo wa wageni, mashabiki, timu na wadau wa michezo kutoka mataifa mbalimbali.

Amesisitiza kuwa maandalizi ya AFCON yanapaswa kuhusisha sekta mbalimbali za uchumi ili fursa zitakazotokana na mashindano hayo zisibaki katika viwanja vya michezo pekee bali ziwafikie wananchi kupitia biashara, huduma, ajira na uwekezaji.

Hatua hiyo inaifanya Tanzania kuwa na nafasi muhimu katika uratibu wa maandalizi ya mashindano hayo baada ya ofisi za uratibu za CAF kuhamishiwa Dar es Salaam kutoka Nairobi, Kenya.

Ofisi hizo zitakuwa kitovu cha kuratibu shughuli mbalimbali kati ya CAF na nchi tatu zitakazokuwa wenyeji wa mashindano hayo.

Uratibu huo utahusisha masuala ya usimamizi wa mashindano, miundombinu, usalama, usafiri, malazi, vifaa, masoko na shughuli za habari na utangazaji.

Hatua hiyo inatarajiwa kuimarisha mawasiliano na ushirikiano kati ya CAF, serikali za nchi hizo pamoja na kamati za maandalizi ili kuhakikisha shughuli zote zinafanyika kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa na shirikisho hilo.

Katika hatua nyingine, uzinduzi huo umeambatana na utiaji saini wa makubaliano ya kimkakati kati ya CAF na TTB yatakayoiwezesha Tanzania kutumia umaarufu wa mashindano hayo kutangaza vivutio vyake vya utalii kimataifa.

Kupitia makubaliano hayo, TTB imepata nafasi ya kuwa mdhamini rasmi (Official Sponsor) wa mashindano ya TotalEnergies CAF AFCON PAMOJA 2027.

Ushirikiano huo unalenga kuitangaza Tanzania kama moja ya maeneo muhimu ya utalii barani Afrika huku ukitumia mvuto wa soka la Afrika kuvutia wageni na uwekezaji.

Akizungumzia makubaliano hayo, Mkurugenzi Mkuu wa TTB, Dkt. Thereza Mugobi, amesema mashindano hayo ni fu.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa CAF Samson Adamu amesema ushirikiano huo ni hatua muhimu katika maandalizi ya AFCON 2027 huku akieleza kuwa ameshuhudia shauku kubwa ya Watanzania kuhusu mashindano hayo.

Adamu pia ameonesha umuhimu wa lugha ya Kiswahili katika shughuli za shirikisho hilo akianza hotuba yake kwa lugha hiyo na kueleza kuwa kwa nafasi aliyonayo ndani ya CAF hawezi kuiepuka lugha hiyo.

Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya CAF kutangaza rasmi kutambua Kiswahili kuwa mojawapo ya lugha zake rasmi hatua iliyofikiwa katika Mkutano Mkuu wa 48 wa shirikisho hilo uliofanyika Abuja, Nigeria, Novemba 21, mwaka huu.

Kiswahili kimeongezwa katika orodha ya lugha rasmi za shirikisho hilo, ambazo ni Kiingereza, Kifaransa, Kiarabu na Kireno.

Uamuzi huo una maana kuwa Kiswahili sasa kinatambuliwa katika shughuli rasmi za kiutawala na mawasiliano ya CAF, hatua inayopanua nafasi ya lugha hiyo katika usimamizi wa soka la Afrika.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya AFCON 2027, Leodger Tenga, amesema Tanzania iko tayari kwa mashindano hayo na imedhamiria kutumia nafasi hiyo kuonesha uwezo wake katika kuandaa matukio makubwa ya kimataifa.

Tenga, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), amesema ni fahari kwa Tanzania kupata jukumu muhimu katika maandalizi ya mashindano hayo na kwamba nchi imejiandaa kuonesha kwa vitendo dhamira yake ya kuleta mageuzi katika sekta ya michezo.