Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky ameishutumu Urusi kwa kutoshiriki kwa dhati kwenye mazungumzo ya amani na kwa kutaka kuendeleza uvamizi wake wa miaka mitatu, licha ya msukumo wa Marekani wa kusitisha mapigano.
Matamshi haya ameyatoa siku moja baada ya Rais wa Marekani Donald Trump, kuzungumza kwa njia ya simu na Zelensky na Rais wa Urusi, Vladmir Putin kuhusu vita hivyo.
Zelensky ameandika katika mtandao wa kijamii kwamba ni dhahiri Urusi inajaribu kupoteza muda kwa lengo la kuendeleza vita vyake na uvamizi wake.
Kulingana na Zelensky, Ukraine iko tayari kwa muundo wowote wa mazungumzo ambao utakuwa na matokeo mazuri.
Alibainisha kuwa ikiwa Urusi itaendelea kuweka mezani madai yanayokwamisha kupigwa hatua, lazima hatua kali zichukuliwe.
Rais huyo wa Ukraine amesema hali hiyo sio tu ilishindwa kufafanua mustakabali wa mazungumzo hayo, bali pia yanaifanya hali kuwa ya kukanganya.
