CHAMA cha ACT-Wazalendo kimelitaka Bunge la Ulaya kuondoa azimio la kutaka kusitishwa kwa mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga.

Msemaji wa Sekta ya Madini katika chama hicho, Isihaka Mchinjita alieleza hayo jana kupitia taarifa kwa vyombo vya habari.

Mchinjita alisema chama hicho kinalaani maazimio ya Bunge la Umoja wa Ulaya kwa kuwa yanaingilia mambo ya ndani ya Uganda na Tanzania na pia ni ukiukwaji wa mkataba wa Umoja wa Mataifa.

“Vitendo hivi vinavyofanywa na Umoja wa Ulaya vinakiuka misingi ya sheria za kimataifa na haki isiyoweza kuondolewa ya watu wa Uganda na Tanzania ya kujiamulia mustakabali wao na mamlaka ya kujitawala, nchi za Kiafrika ni huru, tunakaribisha ushauri wowote mzuri lakini hatutokubali kupokea maagizo na amri kutoka kwa wadau kutoka nje,” alisema Mchinjita.

Alisema ACT-Wazalendo kinasikitishwa na azimio hilo la Septemba 15, mwaka huu lililodai mradi huo utaharibu bayoanuai (viumbehai) na kusababisha mabadiliko ya tabianchi, kitu ambacho siyo kweli.

Kwa mujibu wa Mchinjita, madai hayo ya Bunge la EU yanalenga kuzuia uanzishwaji wa kiwanda cha kusafisha mafuta na kutoa shinikizo kwa wawekezaji watarajiwa kusitisha uamuzi wa mwisho wa kuwekeza mradi huo.

Alisema chama chao kinatambua na kuthamini hatua na juhudi zinazofanywa na wanaharakati wa mazingira, watetezi wa haki za binadamu na asasi nyingine za kiraia (Azaki) za ndani ya nchi zote mbili kuzitahadharisha na kuziwajibisha serikali mbili za Uganda na Tanzania kuzingatia athari za mazingira na kujali haki za binadamu.

Kutokana na azimio hilo, ACT-Wazalendo kimelitaka Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kutoa azimio la kulinda uhuru wa Tanzania na Uganda katika kujiamulia mambo yao na kutaka mazungumzo na Bunge la Ulaya.

By Jamhuri