urlWiki iliyopita familia ya soka duniani imepata pigo, baada ajali ya ndege  iliyosababisha vifo vya watu 81, wakiwamo wachezaji wa klabu ya Chopecoense ya nchini Brazil na kuacha simanzi kubwa

Ndege iliyokuwa imebeba timu ya soka ya Brazil ilianguka wakati ilipokuwa ikikaribia mji wa Medellin nchini Colombia.

Ajali hiyo ilihusisha ndege ya kukodi  ya  Shirika la Liama la nchini Bolivia iliyotengenezwa na Kampuni ya BAe ya nchini Uingereza.

Timu hiyo ilikuwa ikielekea Medellin kucheza dhidi ya klabu Atletico Nacional katika mashindano ya Copa Sudamericana ambayo kwa Afrika ni sawa na michuano ya CAF.

Mikasa mingine inayokumbukwa ni:

 

1949 Il Grande Torino

Mwezi Mei mwaka 1949 ndege iliyokuwa imeibeba timu ya Torino ilianguka eneo la milima karibu na Turin na kuwaua watu 31 timu hiyo ya “Il Grande Torino” ilikuwa klabu kubwa nchini Italia baada ya kupata ushindi mara tano.Klabu hiyo haikuweza kujikwamua kufuatia ajali hiyo ambayo iliangamiza karibu kikosi chote.

 

1958 Ajali ya Munich

Ndege iliyokuwa imebeba timu cha Manchester United ambayo ilikuwa wakati huo ilijulikana kama “the Busby Babes” ilianguka ilipokuwa ikijaribu kupaa, wakati timu ilikuwa ikirudi kutoka mechi ya bara ulaya dhidi ya klabu ya Red Star Belgrade wachezaji 8 wa United na watu wengine 15 waliaga dunia.

 

1961 timu ya kuteleza kwenye theluji ya Marekani

Wachezaji wote 18 wa timu ya kuteleza kwenye theluji ya Marekani walikuwa miongoni mwa watu 73 waliokufa baada ya ndege yao kuanguka karibu na uwanja wa ndege wa Brussels wakati ilipokuwa ikitua.

Timu hiyo ilikuwa safarini kwenda mji wa Prague, huko Jamhuri ya Czech,  kushiri mashindano na dunia ambayo hata hivyo yalifutwa.

 

1972 Old Christians

Siku ya Ijumaa tarehe 13 Oktoba mwaka 1972, ndege iliyokuwa imebeba timu ya Old Christians ya raga ya Uruguay, ilitoweka ilipokuwa safarini kutoka mji wa Montevideo kwenda Santiago nchini Chile.

Miezi miwili baadaye jeshi la wanaanga wa Chile waliwapata manusura 14 kutoka katika ajali hiyo. Wengine wawili walikuwa wametembea kwa siku 10 kabla ya kukutana na wafugaji katika milima ya Andean.

Mkasa huo uliandikwa kwenye vitabu na baadaye kutengenezwa filamu, ALIVE, iliyoeleza jinsi manusura walikula nyama ya binadamu kuepuka kufa njaa.

 

1979 Pakhatakor

Mwezi Agosti mwaka 1979 wachezaji 17 wa timu ya soka la Pakhtakor Tashkent waliuawa wakati ndege yao iligongana na ndege ngingine katika anga ya Ukrain watu wote 178 waliokuwa ndani ya ndege zote mbili walipoteza maisha.

 

1987 Alianza Lima

Timu ya soka ya Alianza Lima, moja ya vilabu vyenye mafanikio makubwa zaidi ilikuwa ikirejea mjini Lima, ndege yao ilianguka baharini dakika chache kabla ya kutua na watu 43 walipoteza maisha katika ajali hiyo huku rubani pekee akinusurika.

 

1993 Timu ya Soka ya Zambia

Wachezaji18 wa timu ya taifa ya Zambia (Chipolopolo), walikufa wakati ndege ya jeshi la Zambia ilipoanguka karibu na Gabon tarehe 28 mwezi Aprili mwaka 1993, kikosi hicho kilikuwa kikielekea kucheza mechi ya kufuzu kwa kombe la dunia nchini Senegal.

 

2011 Lokomotiv Yaroslavl

Timu hiyo  ilikuwa mabingwa mara tatu nchini Urusi ya Lokomotiv Yaroslavl, wachezaji wote walikufa katika ajali ya ndege mwezi Septemba mwaka 2011 huku mabaki ya ndege hiyo yakipatikana kwenye mto na kuacha simanzi. Ndege hiyo ilikuwa ilikuwa ikielekea nchini Belarus kucheza  mechi ya kwanza ya msimu,  wachezaji 36 na maafisa walifariki pamoja na wahudumu 7.

By Jamhuri