Polisi mkoani Songwe limemkamata, Aloyce Nyabwanzo (51), mkazi wa kitongoji cha Kikamba,kijiji cha Kapalala Wilayani, Songwe kwa tuhuma za kuwaua wajukuu zake wawili kwa kuwapasua mafuvu ya kichwa na mchi wa kutwangia mahindi na kusababisha ubongo kumwagika.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Theopista Mallya, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo lilitokea Aprili 30,mwaka huu, majira ya saa 5:00 usiku wilayani Songwe.

Amesema kuwa mtuhumiwa alitumia mbinu ya kuwavizia wajukuu zake hao wakati wakitoka chumbani kwao na kwenda kumfuata bibi yao sebuleni aliyekuwa akizuia mlango usivunjwe baada ya mtuhumiwa kuanzisha vurugu nyakati hizo za usiku.

“Marehemu hao wamefanyiwa uchunguzi wa awali na kubaini kuwa vifo vyao vimesababishwa kupasuka kwa mafuvu baada ya kupigwa na kitu kizito kichwani na kusababisha kuvuja damu nyingi na ubongo kutoka nje” amesema Kamanda Mallya.

Amewataja marehemu hao kuwa ni Jackson Chacha (2) na George Chacha (5) wote wakazi wa kitongoji cha Iwindu- Kikamba katika kijiji cha Kapalala na walikuwa wakilelewa na mtuhumiwa.

Kamanda Mallya amesema wanamshikilia mtuhumiwa huyo na anatarajiwa kufikishwa mahakamani mara baada ya mtuhumiwa kupelekwa hospitali na kupimwa afya ya akili.

By Jamhuri