BODI YA MIKOPO YA ELIMU YA JUU YATANGAZA MSAKO KWA WADAIWA SUGU

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini (HESLB) imesema kuanzia Jumatatu ijayo, Januari 8, 2017 itaanza kukagua taarifa za mishahara za waajiri (payroll) ili kubaini waajiri ambao wanawasilisha kiwango kidogo cha mikopo ya wafanyakazi wao ambao ni wanufaika wa mikopo hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo, Abdul-Razaq Badru amesema wanufaika wengi wa mikopo, wakiwemo wadaiwa sugu, wameonesha ushirikiano mkubwa katika kurejesha mikopo yao, hivyo kurahisisha kazi ya kukusanya madeni ya mikopo hiyo.

Bwana Badru ameongeza kuwa Kiasi cha pesa za wadaiwa sugu kilichoiva na kinachotakiwa kuwasilishwa ni Tsh. bilioni 285 ambazo ni madeni ya mikopo iliyotolewa na bodi hiyo tangu kuanzishwa kwake.

Hata hivyo, Badru amesema wamelazimika kufungua ofisi zao nchi nzima kwa ajili kusimamia malipo ya fedha hizo za mikopo, hasa wale waliotajwa kwenye orodha ya wadaiwa sugu ambapo wamewasambaza wakaguzi nchi nzima, kwa ajili ya kufuatilia waajiri wasiotekeleza wajibu wao wa kuwakata asilimia 15 wanufaika hao waliowaajiri.

Badru pia amewasisitiza watu wote waliowahi kukopa, kulipa wenyewe kwa hiyari kwani bila hivyo, watajikuta wakiingia matatizoni na njia pekee inayoweza kumuokoa mtu aliyekopa asilipe, nio kifo.