Na Isri Mohamed

Mwili wa Makamu wa Rais wa Malawi, Saulos Chilima na watu wengine tisa imepatikana baada ya vikosi vilivyokuwa vikiitafuta ndege iliyowabeba kufanikiwa kupata ndege hiyo huku wakiwa wamefariki.

Baada ya kuthibitishwa kwa taarifa hiyo, Rais wa Malawi, Lazarus Chakwera amelihutubia Taifa na kusema ndege hiyo ilianguka katika eneo la Msitu wa Chikangawa huko Mzimba.

Ndege hiyo ambayo ni mali ya Jeshi la Ulinzi la Malawi ilitoweka kwenye rada baada ya kuondoka katika mji mkuu wa nchi hiyo Lilongwe hapo jana asubuhi.

Ilitakiwa kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mzuzu, Kaskazini mwa nchi hiyo baada ya saa nne asubuhi kwa saa za Malawi, lakini haikuonekana.

Makamu huyo wa Rais wa Malawi alikuwa akielekea kuiwakilisha Serikali katika mazishi ya Waziri wa zamani wa Malawi, Ralph Kasambara, aliyefariki dunia siku chache zilizopita.