Rais Magufuli akifurahia jambo na Dkt. Slaa.

 

RAIS Dkt. John Magufuli amempongeza Balozi mteule Dkt. Wilbrod Slaa kwa moyo wake wa kizalendo wa kukubali kwenda kuiwakilisha nchi ya Tanzania katika taifa ambalo atapangiwa muda wowote kutoka sasa huku akijivunia kuwa hakukosea kumchagua yeye (Dkt Slaa)

Magufuli akiagana na Slaa.

 

Rais Magufuli ameeleza hayo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo  na Balozi Mteule Mhe. Dkt. Wilbrod Peter Slaa, Ikulu Jijini Dar es Salaam na kusema aliamua kumteua kuwa Balozi kwa kuwa anatambua ataweza kupigania maslahi ya Tanzania popote atakapopangiwa kuiwakilisha.

Dkt. Slaa alinijulisha kuwa anakuja na akaomba akija angependa kuja kuniona na nikampangia leo, tumezungumza mambo mengi na ameniahidi kuwa atakwenda kufanya kazi yake vizuri kwenye nchi atakayokwenda kuwa Balozi. Dkt. Wilbrod Slaa ni mtu safi, anazungumza kutoka moyoni na anaipenda Tanzania na mimi kutokana na moyo wake wa kuchukia ufisadi na kuchukia wizi nikaamua kumteua kuwa Balozi. Kwa hiyo sikukosea kumchagua”, alisema Rais Magufuli.

 

Rais Magufuli akimkaribisha Slaa Ikulu.

 

Kwa upande wake Dkt. Slaa amempongeza Rais Magufuli na Serikali yake ya Awamu ya Tano kwa uongozi bora wenye maono na uthubutu wa kutekeleza mambo makubwa yenye maslahi kwa nchi ikiwemo miradi mikubwa kama vile ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge), ujenzi wa daraja la juu (Flyover) katika makutano ya barabara ya Nyerere na Mandela (Tazara), mradi wa uzalishaji umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stieglers’ Gorge) na mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi.

“Kwa kweli naona faraja, ninafurahi Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza hatua kwa hatua karibu yote tuliyokuwa tunayapigania kwa miaka takribani 20 ya huko nyuma, na mimi Dkt. Slaa nilikuwa napiga kelele kwa sababu nilikuwa naona kuna upungufu”, alisema Dkt. Slaa.