


Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Joyce Ndalichako amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imedhamiria kutatua changamoto za wafanyakazi ili kuboresha maslahi yao.
Waziri Ndalichako ametoa kauli hiyo jana wakati akifungua semina ya siku moja kwa Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) kuhusu uelewa wa Kanuni mpya ya mafao ya pensheni katika ukumbi wa PSSSF, jijini Dodoma.
Amesema kuwa, Rais Samia anawajali na kuwathamini wafanyakazi kutokana na mchango wao mkubwa wanaotoa katika ujenzi wa uchumi wa nchi na ndio maana anataka kila mtumishi aweze kushiriki kikamilifu katika kukuza maendeleo ya nchi.
“Ninyi nyote ni mashahidi katika kipindi cha uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan watumishi wameweza kupandishwa madaraja vilevile ajira zimetangazwa kwa wingi katika sekta mbalimbali ikiwemo Afya, Elimu”
“Nimshukuru Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan kwa kufanya uamuzi wa kulipa shilingi trilioni 2.17 kwa ajili ya kulipa deni lililodumu kwa muda mrefu la shilingi trilioni 4.6 la michango kabla ya 1999 kama malipo ya deni la Serikali kwa lengo la kukomboa mifuko,”
Aidha, Waziri Ndalichako ametumia fursa hiyo kuwasisitizia viongozi hao wa Vyama vya Wafanyakazi juu ya umuhimu wa kuendelea kutoa na kueneza elimu hiyo ya Kanuni mpya ya mafao ya pensheni iliyoanza kutumika Julai 1, 2022 kwa wanachama nchi nzima.
Sambamba na hayo, Mhe. Ndalichako amewataka viongozi hao kuendelea kushirikiana na Serikali ili kuleta tija na ufanisi katika kukuza sekta ya kazi na ushughulikiaji wa masuala ya wafanyakazi nchini.
Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA), Tumaini Nyamhokya amesema kuwa semina hiyo itasaidia kuwajengea uelewa viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi juu ya Kanuni hiyo mpya ya mafao ya pensheni, ili waweze kukuza uelewa wa wanachama kuhusu kanuni hiyo kwa wanachama wengine.
WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ,kupitia shamba la miti la Sao Hill lilopo wilaya ya Mufindi mkoani Iringa wamefanikisha mashindano ya magari ya mbio fupi ya Sao Hill Auto Cross ambayo yalikuwa kivutio kikubwa kwa wananchi wa mkoa wa Iringa na nje ya mkoa wa Iringa waliofika katika eneo ambalo mashindano yalifanyikia
Akizungumza baada ya kuzinduliwa rasmi kwa mashindano hayo katika Shamba la Miti Sao Hill linalomikiliwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS), Mhifadhi Mkuu wa Shamba hilo Lucas Sabida amesema ndio mara ya kwanza kwa Wakala huo kuandaa mashindano hayo ikiwa ni utalii mpya ambao wameutambulisha kwenye sekta ya utalii nchini.
“Katika shamba la Sao Hill fursa ziko nyingi , tunazalisha bidhaa zinatokana na mbao , asali na tunazo fursa za uwekezaji.Sasa tumekuja na utalii wa michezo kwenye maeneo yetu ya hifadhi za misitu ya asili na ile misitu ya kupanda kama Sao Hill kama ambavyo leo tumeanza na mbio fupi za magari.
“Sao Hili tunalo eneo lenye ukubwa wa zaidi ya hekta 155,000 na zina barabara zenye urefu wa kilometa 1,500 kwa hiyo ukiunganisha hizi barabara unaweza kutoka hapa(Sao Hill) hadi Mwanza .Hivyo tunaweza kufanya mashindano makubwa ya ya magari hata ya Bara la Afrika,”alisema.
Ameongeza katika shamba la Miti Sao Hill inawezekana kufanyika michezo ya aina yoyote kwani kuna eneo kubwa na la kutosha lakini TFS wameamua kuanza na mashindano ya magari ambayo wanatarajia yatakuwa yakifanyika kila mwaka kwa kushirikiana na wadau wengine.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Saad Mtambule mkoani Iringa alisema utalii wa mashindano ya mbio za magari kwenye Shamba la Sao Hill unakwenda kufungua fursa zaidi katika sekta ya utalii na wao wamejiandaa kupokea wananchi na wawekezaji walio tayari kufanya uwekezaji kwenye sekta ya utalii.
Alisema sekta hiyo imeendelea kukua kwa kasi kubwa kutokana na jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan tangu alipotangaza utalii kupitia filamu ya Royal Tour.
“Tunamshukuru Rais Samia kwa kuanzisha filamu ya Tanzania Royal Tour na sisi kupitia sekta ya misitu tumeona pamoja na kupata mbao na kutengeneza bidhaa mbalimbali zitokanazo na misitu tunaamini mashindano ya magari yataongeza fursa na kuleta bidhaa mpya kwenye sekta ya misitu .
“Pia tunawapongeza TFS kupitia Shamba la Miti Sao Hill pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii ikiongoza na Balozi Pindi Chana kwa uratibu mzuri wa mashindano haya ya magari yanayofanyika hapa. Kwetu mashindano haya ya magari yanakwenda kuongeza fursa nyingine kwa wananchi wetu,”amesema.
Kwa upande wa Mchezeshaji wa Mbio hizo za magari John Makeo alisema mashindano hayo yamefanyika ya kilometa sita na kila mzunguko ulikuwa ni kilometa 1.5.“Mbio fupi lengo lake ni kuwaanda madereva wa kesho na keshokutwa , kikatiba mbio hizo zinatakiwa kuchezwa kilometa moja, isizidi kilometa 1.5.”
Aidha alisema Sao Hill kuna maeneo mazuri kwa ajili ya kufanya mashindano ya mbio za magari hasa kwa kuzingatia kuna eneo la kutosha na bahati nzuri hakuna makazi ya watu zaidi ya msitu ulitokana na miti ya kupandwa na miti asili
Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Dar
SHERIA ya habari ya mwaka 2016 ilianza kulalamikiwa kwa kipindi kirefu na wadau wa habari kwa kuwa haikuondoa mitego iliyowekwa na sheria ya mwaka 1979 na kuchangia kudumaa kwa vyombo vya habari nchini.
Hayo yamesemwa leo na Neville Meena ambaye ni mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),Septemba 13, 2022 wakati akizungumza katika Kipindi cha Front Page kinachorushwa na Radio +255 Global jijini Dar es Salaam.
Meena amesema kuwa sheria hiyo ilianza kupigiwa kelele kwa muda mrefu na wadau wa habari ambapo Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan iliona haja ya kukaa meza moja na wadau wa habari ili kuipatia ufumbuzi.
Amesema, hatua za awali alizochukua Rais Samia Suluhu Hassan,ziliongeza ari ya wadau wa habari kushirikiana ili kung’oa vipengele hasi vya sheria ya habari.
‘‘Hatua zilianza kuchukuliwa kwa serikali kuleta mapendekezo ya maeneo ya kurekebisha, lakini na sisi tuliongeza yetu ambayo wao walikuwa hawajaweka kwenye mapendekezo yao kwa kuwa mabadiliko hayo yalianzia kipengele cha 38.
“Sheria ya Habari ya Mwaka 1976, imefanya kazi kwa miaka 40, muda wote huo imetoa mwanya kwa mtu mmoja (waziri) kufungia chombo cha habari anapojisikia kufanya hivyo.
“Hata Sheria ya Habari ya Mwaka 2016 ilipotungwa, imefuata mkondo huo huo wa kutoa mamlaka kwa mtu mmoja kuamua kufungia chombo cha habari ama la ingawa mamlaka hayo amepewa Mkurugenzi wa Idara ya Habari Malelezo.Katika mabadiliko haya, tumeiomba serikali iondoe kipengele hicho,’’amesema Meena.
Hata hivyo Mei 2,202 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan alielekeza Sheria za Habari ambazo zimekuwa zikilalamikiwa kubinya uhuru vya vyombo vya habari nchini zirekebishwe.
Rais Samia alitoa maelekezo hayo wakati akiwahutubia Wadau wa Vyombo vya Habari kwenye maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari
ikiongozwa na kauli mbiu ‘Uandishi wa habari na changamoto za kidigiti’katika ukumbi wa Gran Melia Hotel jijini Arusha.
“Nimeelekeza Sheria zirekebishwe, lakini kwa majadiliano pande zote na si tu kwamba sisi tunataka nini. Nimemwelekeza Waziri sheria za habari zirekebishwe kwa kushirikisha wadau wote,”aliagiza Rais Samia
Naye Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye wakati akihojiwa na BBC alisema kuwa,wanaingia hatua ya pili na wadau wa habari ili pale ambapo hawakukubaliana waweze kujadili kupata mwafaka kwa hatua zaidi.
“Nimeletewa ripoti ya majadiliano yale, tunakwenda hatua ya pili sasa kule ambako walishindwa kukubaliana, tunataka tuongeze kikao kingine tukajadili yale tu ambayo hatukukubaliana.
Lakini, niwahakikishie wadau wa habari kwamba, hatutaenda bungeni bila kukubaliana,lazima tukae tukubaliane, tushauriane tufikie mwisho,”.
“Hatutaki kutunga sheria kesho na kesho kutwa tukarudi tena kwenda kurekebisha, na ndiyo maagizo ya Mheshimiwa Rais Samia (Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan) kwamba tukae tuzungumze, tujadiliane mpaka tukubaliane
Na Mwandishi Wetu,JamhuruiMedia,Mwanza
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Kanali Mstaafu Abdulrahman Kinana, amesema Chama kinaridhishwa na mwenendo wa ujenzi wa daraja la JPM Magufuli linalounganisha kati ya Mkoa wa Mwanza na Geita ambalo linajengwa eneo la Kigogo-Busisi.
Akizungumza wakati akikagua daraja hilo Kinana ambaye yupo katika ziara ya kukagua uhai wa Chama na kuangalia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025, amesisitiza daraja hilo ujenzi wake unakwenda kwa wakati kama ilivyopangwa, hivyo mwaka 2024 nchi itakuwa imepata alama kubwa ya kuwa na daraja refu lenye urefu wa karibu kilomita 3.2.
“Najaribu kukumbuka madaraja mangapi katika Afrika yenye urefu huo kama hili halitwakua la kwanza basi litakuwa katika tatu bora. Hivyo niwapongeze wote wanaoshiriki ujenzi wa daraja hili ndugu zetu wa kutoka Korea, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wajenzi kutoka Kampuni ya China na Watanzania wote wanaoshiriki,” amesema Kinana.
Kinana akiwa kwenye daraja hilo baada ya kulikagua na kupata maelezo ya ujenzi wake ambao umefikia asilimia 51, amepata nafasi ya kuwasilimia wajenzi wa daraja hilo na kuwapongeza kwa kazi nzuri.
“Mnafanya kazi nzuri sana, mnafanya kazi kubwa na Rais (Samia Suluhu Hassan) ametumina nije niwasalimie na niwambie kwamba anangojea aje kuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa daraja hili litakapokamilika,” amesema Kinana.
Awali Mhandishi Mshauri wa ujenzi wa daraja hilo Abulkarika Majuto ameelezea hatua kwa hatua kuhusu ujenzi huo ambapo amesema kwa sasaa umefikia asilimia 51.
“Tunakukaribisha kwenye ujenzi wa daraja la JP Magufuli ambalo lina urefu wa kilomita 3.2 pamoja na barabara unganishi za kilomita 1.66 na kwamba daraja hili litakapokamilika litaziunganisha wilaya mbili za Sengerema na Misungwi ambazo zinatenganishwa na Ziwa Victoria kwa kupitia barabara ya kupitia Usagara, Sengerema hadi Geita.
“Barabara hii ya Usagara, Sengerema hadi Geita ni miongoni mwa barabara ambazo zinapita katika ukanda huu wa Ziwa Victoria na utekelezaji wake ni miaka minne ambapo unatarajia kukamilika Februari 24, mwaka 2024.
Na Munir Shemweta,JamhuriMedia, Kibaha
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabuka amewataka wananchi wote wanaonunua ardhi kufanya uhakiki kabla ya kununua kupitia ofisi za Halmashauri sambamba na kufanya Search kwa maeneo yaliyo na hati.
Dkt Mabula amesema hayo wilayani Kibaha tarehe 1 Sept 2022 wakati alipokwenda na Waziri wa Uvuvi na Mifugo Mashimba Ndaki kupokea na kukabidhi taarifa ya uchunguzi wa mgogoro wa ardhi katika eneo la kiwanja namba 34 Pangani Kibaha chenye ukubwa wa hekta 1037 ambapo wananchi 1002 wamebainika kuvamia kiwanja cha eneo hilo linalomilikiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi chini ya taasisi yake TVLA ,
Katika uchunguzi wake, Kamati ilifanikiwa kuwahoji wananchi wavamizi 1,156 katika
mitaa ya Kidimu, Lumumba na Mkombozi na kuwasikiliza, kuwahoji na kupokea vielelezo mbalimbali kutoka kwa wananchi wavamizi 1002 ambapo wavamizi 154 hawakuwa na nyaraka zozote za namna walivyopata maeneo kwenye eneo hilo.
Akisoma taarifa ya Kamati ya uchunguzi, Katibu wa Kamati ambaye ni Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Pwani Husein Sadick, amesema katika mahojiano na wananchi hao, 403 walikiri kuvamia kwa kujikatia vipande vya ardhi, 46 walidai kupewa vipande vya ardhi na wavamizi waliotangulia na wananchi 6 walidai walirithi maeneo hayo. Hata hivyo, wavamizi hao wamefanya maendelezo pasipo kupata kibali cha ujenzi kutoka Halmashauri kama taratibu zinavyoelekeza.
Kwa mujibu wa Husein Sadick, historia ya eneo hilo ilianza 1982 kwa Wizara kuomba eneo la kuzalisha mitamba kwa ajili ya kuhudumia kanda ya mashariki na hekta 4000 kutwaliwa huku wananchi waliokuwa wakiishi eneo hilo walilipwa fidia kwa awamu tofauti.
“Eneo lilipatikana kihalali na wizara na mwaka 2007 wananchi walivamia ambapo tathmini ya kamati ilibaini uwepo nyumba zilizojengwa kwa tope au mabati, nyumba zisizokamilika au chumba kimoja pamoja na zile zenye makazi” amesema Husein Sadick.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa mtaa wa Lumumba kata ya pangani Kibaha mkoani Pwani Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alitoa rai kwa wananchi wote wanaonunua ardhi kufanya uhakiki kabla ya kununua kupitia ofisi za Halmashauri na kufanya Search kwa maeneo yaliyo na hati.
‘’Nitoe rai kwa wananchi wote wanaonunua ardhi kufanya uhakiki kabla ya kununua kupitia ofisi za Halmashauri na kufanya Search kwa maeneo yaliyo na hati’’ amesema Dkt.Mabula
Akielezea mgogoro katika eneo la Pangani, Waziri wa Ardhi alieleza kuwa, katika eneo hilo ilibainika uwepo wa wavamizi waliounda magenge ya kutapeli wageni kutoka nje ya Kibaha hasa kutoka Mkoa wa Dar es Salaam na kujifanya wamiliki wa asili katika maeneo waliyovamia.
Hata hivyo, Waziri wa Ardhi alielekeza wananchi wote waliouziwa ardhi ndani ya Kiwanja Na. 34 Pangani kuwafungulia mashtaka ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu wale wote waliowauzia ardhi pamoja na walioshirikiana nao kufanya mauzo hayo.
Pia alitaka wavamizi wote waliotumia/kuandaa nyaraka za kughushi wachukuliwe hatua za kisheria kwa kusababisha uvamizi kwenye maeneo yenye miliki za watu wengine.
Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki alisema, amefurahi mgogoro wa ardhi kati ya wananchi na taasisi iliyo chini ya wizara yake mefikia mwisho na kuishukuru wizara ya ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuunda tume ya kuchunguza suala hili.
“Naipongeza timu ya uchunguzi kwa kueleza ukweli na ukweli unapendwa na watu wachache na nakubaliana na mapendekezo yote ya timu ya uchunguzi” alisema Ndaki.
Ndaki amesema, Wizara yake ina huruma sana maana pamoja na kumiliki kihalali helta zote 4000 lakini bado imeamua hekta 2,963 kati ya hizo ziende halmashauri na wao kubaki na hekta 1,137.
Hata hivyo, Ndaki ameagiza kuchukuliwa hatua kwa yeyote atakayevamia tena eneo lililobaki huku akisisitiza mipaka ya eneo lililobaki ianishwe na kulindwa ili kuepuka uvamizi mwingine.
Mkuu wa mkoa wa Pwani Alhaji Abuubakar Kunenge amesema, uongozi wa mkoa wake utasimamia na kutenda haki wakati wa utekelezaji mapendekezo ya tume ya uchunguzi na kusisitiza haki itendeka.
“Katika kushughulikia utekelezaji mapendekezo ya kamati haki itatendeka na anayestahili watamlinda na asiyestahili atupishe na hakuna atakayenyang’anywa haki yake” amesema Kunenge.
Mkoa wa Pwani umekuwa na migogoro mingi ya ardhi ambapo Waziri wa Ardhi aliunda Kamati ya Uchunguzi kubaini namna wavamizi walivyopata ardhi, kubaini matapeli wote waliohusika kuuza ardhi na kisha kuishauri Serikali hatua stahiki za kuchukua.