Chadema Kukutana, Kuzungumza Yanayoendelea Nchini

Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) itakutana katika kikao cha dharura, kwa mujibu wa Katiba ya Chama, siku ya Jumatano, Desemba 6, mwaka huu, jijini Dar es Salaam.

Katika kikao hicho cha siku moja, pamoja na masuala mengine, Kamati Kuu ya Chama itapokea na kujadili agenda ya Mwenendo wa Hali ya Kisiasa nchini, kipekee kuhusu;

i.Taarifa na tathmini ya uchaguzi mdogo wa udiwani kata 43.

ii. Uchaguzi wa mdogo wa ubunge katika majimbo 3 na kata 6.

Kupitia taarifa hii pia, chama kimepokea kwa tahadhari taarifa za ‘kupotea’ kwa Mwandishi wa Habari wa Mwananchi Communication Ltd, Azory Gwanda.

Chama kinalaani vikali tukio hilo kwa sababu hadi sasa linadhaniwa kuwa na mazingira ya mwendelezo wa vitendo na matukio ya utekaji na mengine vya namna hiyo, ambayo yalianza kwa wanasiasa na wasanii na sasa yanaanza kujitokeza pia kwa waandishi wa habari. Tunalitaka Jeshi la Polisi nchini kuhakikisha linamaliza utata wa kutookena kwa mwandishi huyo.

Wajibu namba moja kwa serikali yoyote ile makini ni kulinda raia wake. Vyombo vya dola vyenye wajibu wa kulinda raia na mali zao, vinalo jukumu la kuchukua hatua, kupata majibu ya kumaliza sintofahamu hii inayozidi kulikumba taifa; ya watu kupotea, kutekwa, kushambuliwa kwa nia ya kuuwawa na kuokotwa kwa miili ya watu wakiwa wamekufa.

Matukio haya yakiachwa bila kutafutiwa ufumbuzi wa haraka na kuyamaliza kabisa, tutakuwa tumeruhusu dalili mbaya kabisa za tishio la usalama wa raia mmoja mmoja, mali zao na hatimae jamii nzima.

Imetolewa leo, Jumanne, Desemba 5, 2017 na;
Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA