Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila amesema TASAF imekua mkombozi mkubwa wa kuondoa umasikini katika Jamii watu wengi wamebadili maisha yao, pia ni ukweli usiopingika kati ya programu nyingi zilizoanzishwa kwa lengo la kupunguza umasikini miongoni mwa jamii TASAF ni ya mfano.

Albert Chalamila ameyasema hayo mapema leo Dsemba 22, 2023 katika kikao cha tathmini cha utekelezaji mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) kilichofanyika katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam.

RC Chalamila alisema TASAF imekuwa msaada mkubwa sana katika kuboresha kaya maskini kwenye nyanja anuai kama vile huduma za elimu, afya na kuinua watu kiuchumi hivyo TASAF inatakiwa kuwafikia walengwa wengi zaidi waliokusudiwa.

Pia RC Chalamila amewaasa waratibu na wataalam wengine wa TASAF kuwajengea utambuzi wanufaika wao kwa kuwa pesa hazikamilishi maisha ya mwananadamu na kuna wengine wanatakiwa kunufaika, “Kama mtoto atapata ajira, akaajiriwa halafu akaruhusu mzazi wake aendelee kuwa kwenye TASAF maana yake kijana huyo anahitaji viboko mbele ya mzazi wake.”

Vilevile RC Chalamila alisema kuna muhimu kwa wanafaika wahusishwe katika vikao kama hivyo ili wapate kujua kinachoendelea na aliwahimiza viongozi wawe na nidhamu za kiutumishi na pesa zinazotolewa zipelekwe kwa walengwa hayo ndio matarajio ya Mhe Rais Dkt Samia Suluhu na sio vinginevyo.

Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa DSM, Bi. Rehema Madenge alisema ni wajibu wa kila mmoja kupambana na changamoto ili walengwa wa TASAF  wanufaike inavyotakiwa.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Uratibu, Bi. Haika Shayo naye alisema ushauri na maagizo yaliyotolewa kupitia kiako hicho  watayafanyia kazi ili kuboresha mfumo huo kwa walengwa wao.

By Jamhuri