Na Daniel Limbe, JamhuriMedia,Chato

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewahakikishia wananchi wa wilaya ya Chato mkoani Geita kuwa ujenzi wa tawi la Chuo kikuu cha UDSM kitivo cha slSayansi ya Uvuvi (Institute of Marine Science) kinaendelea kujengwa kwenye kijiji cha Kasagara kama yalivyokuwa maono ya Hayati Rais Dk. John Magufuli.

Majaliwa ameyasema hayo leo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya stendi ya zamani ya mabasi Chato mjini, ambapo amewataka wananchi kuendelea kuiamini serikali ya awamu ya sita chini ya rais Dkt. Samia Suluhu, na kwamba miradi yote iliyoanzishwa na Hayati rais Dk.Magufuli kwenye wilaya ya Chato lazima itakamilika kama ilivyokusudiwa.

Amesema ujenzi huo ni muhimu sana kwa wananchi wa kanda ya ziwa ambapo kuna idadi kubwa ya wananchi wanaoendesha maisha yao kwa kutegemea shughuli za uvuvi ndani ya ziwa Victoria.

“Lengo la ujenzi wa chuo hiki ni kutoa fursa kwa wananchi wa ukanda wa ziwa kuongeza maarifa na ujuzi katika shughuli za uvuvi endelevu na tayali ujenzi wake umeanza kule Kasagara” amesema.

Kauli hiyo imeonekana kujibu malalamiko yao wananchi hao ambayo pia yawasilisha mwaka jana kwa aliyekuwa Katibu wa Siasa, Itikadi na Uenezi CCM, Paul Makonda,baada ya kufanya ziara ya kikazi wilayani humo na kusikiliza kero mbalimbali za wananchi kwenye mkutano wa hadhara.

Aidha Majaliwa, amemuagiza mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo,Mandia Kihiyo, kuhakikisha anaweka taa za barabarani kwenye barabara zote za mjini Chato ili kudhibiti vitendo vya kiharifu kwa jamii na kwamba miradi huo ukamilike haraka kabla ya kurudi kwenye ziara nyingine wilayani humo.

Kadhalika ametumia fursa hiyo kuwaonya wanaume wote wenye tabia ya kufanya ngono na wanafunzi na kwamba sheria imeboreshwa kwaajili ya wale watakaothibitika kuwapa mimba wanafunzi na kukatisha masomo yao.

Amesema kwa karne hii ni aibu kwa wazazi kuendelea kukatisha masomo watoto wao kwa madai ya kwenda kuchunga ng’ombe na kwamba suala hilo halipaswi kuendelea na kwamba kama ni shughuli za nyumbani zifanyike siku za mapumziko ya jumamosi na Ijumapili ili kutoa fursa kwa watoto kuendelea na masomo yao.

Katika ziara ya siku mbili ya Waziri mkuu kwenye mkoani wa Geita,imehitimishwa wilayani Chato kwa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa soko kubwa la kisasa linalojengwa kwenye mwalo wa Chato Beach na kisha mkutano wa hadhara kwa wananchi wa wilaya hiyo.

Kadhalika Majaliwa ameahidi kurejea tena mkoani humo,ili kukagua miradi ya maendeleo kwenye wilaya ya Mbogwe, Bukombe, Geita mji na halmashauri ya wilaya ya Geita pamoja na Chato hatua itakayosaidia kusikiliza kero za wananchi na kuzipatia ufumbuzi wa kudumu.