Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

SHAHIDI wa upande wa mashitaka Kiran Lalit Ratilal, ameshindwa kutoa ushahidi katika kesi ya kujeruhi inayowaabili wanandoa Bharat Nathwan (57) na Sangita Bharat (54), kwa sababu wakili wa utetezi katika kesi hiyo yupo Mahakama ya Rufani kwenye shauri lingine.

Wanandoa hao ambao ni raia wa Tanzania wenye asili ya kihindi wanaoishi Mtaa wa Mrima – Kisutu, jengo la Lohana Dar es Salaam wanaotuhumiwa kwa mashitaka manne likiwemo la kujeruhi waliyoyatenda Julai 21,2023 kinyume cha sheria.

Kesi hiyo ililetwa Jumatatu tarehe 3 Juni mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa kwa mashahidi wa upande wa mashtaka, mashahidi watatu wameshatoa ushahidi wao.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Mwanga alidai kuwa wana shahidi mmoja na wapo tayari kuendelea na ushahidi, baada ya kudai hayo, upande wa utetezi ulidai kuwa ni kweli kesi ipo kwenye hatua ya ushahidi, lakini kwa bahati mbaya siku ya ijumaa walipata barua kutoka Mahakama ya Rufaa.

“Ni kweli kesi imekuja kwa kusikilizwa, lakini kwa bahati mbaya siku ya ijumaa tulipokea barua kutoka Mahakama ya Rufaa, kwa hiyo wakili ameenda huko,”alidai Wakili Mwanaisha Mshobozi.

Baada ya Mshobozi kudai hayo, Wakili Mwanga alidai kutokana na maombi hayo hawana pingamizi, wanaomba wapangiwe tarehe nyingine ya usikilizwaji ambayo alipendekeza iwe Julai, mwaka huu ambapo hakimu alisema ni mbali sana.

Hakimu Lyamuya aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 25, 2024 kwa ajili ya usikilizwaji, ambapo shahidi Kiran Lalit alionywa na mahakama kufika tarehe hiyo kwa ajili ya kutoa ushahidi.

“Shahidi kwa bahati mbaya Wakili wa washtakiwa hayupo, tumeelezwa hapa yupo Mahakama ya Rufani, unatakiwa tarehe tutakayopanga uwepo mahakamani,”alisema Hakimu

Awali, Fundi Seremala, Dominic Mpakani (43) aliileza mahakama jinsi mshitakiwa Bharat Nathwan allivyomshambulia jirani wake, Lalit Ratilal kwa kumpiga kichwa kifuani kisha akadondoka chini na nakupoteza fahamu kwa muda.

Aidha, alidai kuwa kulikuwa na ugomvi kati ya mke wa Bharat (Sangita Bharat) na mke wa Lalit, (Kiran) ambao walikuwa wakirushiana maneno kwa ukali kwa lugha ya kihindi huku, baada ya muda kidogo waume zao walifika kwa pamoja na kuingilia ugomvi huo.

Alidai kuwa Julai 21,2023 alikuwa nyumbani kwa Lalit Ratilal maeneo ya mtaa wa Mrima katika jingo la Lohana, alimuita kwa ajili ya kuifanyia kazi zinazohusiana na mbao na kazi zingine ndogo ndogo.

Alidai kuwa alifika katika jengo hilo saa tatu asubuhi ambapo bosi wake huyo anakaa floor ya tatu, wakati anaendelea na kazi alidai kuwa Sangita alikuwa amesimama kwenye mlango lake na Kiran alikuwa amesimama kwenye mlango wake, ambapo Sangita Bharat alianza kuzungumza kwa ukali na kwa jaziba akitumia lugha ya kihindi.

“Lakini nilimsikia mke wa Bharat, Sangita akimwambia mke wa Lalit kwamba uchafu wake apeleke huko ambapo vitu vyote vilikuwa vimewekwa katika eneo la Lalit na hakuna kitu chochote kilichokuwa katika eneo la Sangita. Baada ya dakika kadhaa sijui walipiga simu au vipi waume zao walikuja kwa wakati mmoja na malumbano ya maneno yakaendelea kwa wote wanne,” alidai Fundi Mpakani

Shahidi huyo alidai kuwa, wakati malumbano ya maneno hayo yanaendelea wote walikuwa wamesimama kwenye mlango wa Lalit, baada ya muda Bharat akampiga kichwa Lalit na Lalit akadondoka chini na kupoteza fahamu.

Nathwani na mke wake Sangita wakiingia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo kusikiliza kesi ya kujeruhi inayowakabili ya kuwajeruhi jirani zao

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, washitakiwa hao ambao ni raia wa Tanzania jinsia ya kihindi wanaoishi Mtaa wa Mrima – Kisutu, jingo la Lohana Dar es Salaam wanaotuhumiwa kwa mashitaka manne waliyoyatenda Julai 21,2023.

Katika shitaka la kwanza la kujeruhi linalomkabili Nathwani peke yake, ambapo anatuhumiwa Julai 21,2023 akiwa eneo la mtaa wa Mrima-Kisutu, jingo la Lohana, ndani ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam kinyume cha sheria alimsababishia madhara makubwa Kiran Lalit kwa kuzamisha kichwa chake kwenye ndoo la saruji iliyochanganywa.

Pia, katika shitaka la pili la shambulio la mwili linalomkabili Nathwani peke yake, ambapo tarehe hiyo na eneo hilo alimsababishia madhara Lalit Ratilal katika mwili wake kwa kumpiga kichwa, ngumi na mateke kichwani.

Ilidaiwa kuwa katika shitaka la tatu na la nne linalomkabili Sangita peke yake, ambapo anatuhumiwa kutoa matusi makubwa dhidi ya Lalit na Kiran kitendo ambacho kilileta fujo kwa namna ambayo inaweza kuleta uvunjifu wa amani.