Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Daktari bingwa wa maradhi ya moyo wa hospitali ya Shifaa iliyoko Msese Kinondoni jijini Dar es Salaam, Lulu Mageta amewataka vijana kupima afya zao mara kwa mara kwani wengi kwa sasa wanakabiliwa na maradhi ya shinikizo la damu.

Amesema zamani ilionekana kuwa watu wazima ndio wako kwenye hatari ya kupata maradhi ya shinikizo la damu lakini kwa sasa vijana wengi chini ya miaka 40 wanasumbuliwa na tatizo hilo.

Dk Lulu aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumzia ongezeko la magonjwa ya moyo hasa kwa vijana waliochini ya miaka 40 na punguzo lililotolewa na hospitali hiyo kwa vijana wanaotaka kuchunguzwa afya ya moyo.

Alisema vijana nao wanatakiwa kujenga utamaduni wa kupima afya ya moyo mara kwa mara kujua afya zao badala ya kusubiri mpaka hali inapokuwa mbaya ndipo waende hospitali.

“Zamani ilionekana kuwa maradhi ya shinikizo la damu yanawashambulia watu wazima sana pekee lakini kutokana na kubadilika kwa mtindo wa maisha watu wengi hawafanyi mazoezi kwa hiyo vijana wengi kwa sasa wanasumbuliwa na shida kama hiyo,” alisema Dk Lulu na kuongeza

“Tusiendelee kuwa na mawazo yale yale ya zamani kwamba shinikizo la damu ni kwa wazee kwa sababu vijana wengi wanakufa ghafla kutokanana magonjwa haya, tubadili mtindo wa maisha na tufanye mazoezi,” alisema

Aidha, alisema zamani haikuwa rahisi kumkuta kijana wa chini ya miaka 40 akisumbuliwa na maradhi ya moyo lakini miaka ya hivi karibuni imekuwa kawaida kabisa kuwaona vijana wa rika hilo wakisumbuliwa na moyo.

“Uzoefu wa hivi karibuni unaonyesha dhahiri namna vijana wengi wanavyosumbuliwa na shinikizo la juu la damu na maradhi ya kisukari ambayo pia yanasababisha shinikizo la damu, “ alisema

Alisema miongoni mwa sababu za ugonjwa wa shinikizo la damu ni pamoja na kuwa na uzito wa kupindukia na kukaa muda mrefu kwenye maeneo ya kazi bila kufanya mazoezi.

Dk. Lulu alitaja baadhi ya dalili za ugonjwa huo kuwa ni maumivu chini ya moyo, kuchoka kusikokuwa kwa kawaida na mapigo ya moyo kwenda haraka kuliko ilivyokuwa kawaida.

“Ukiona unatembea umbali mdogo tu unachoka sana, umbali ambao zamani ulikuwa unatembea bila shida basi ujue umeanza kupata shinikizo la damu na ugonjwa huu hauji ghafla kama baadhi yetu tunavyodhani unachukua muda mrefu ndiyo maana tunashauri kupima mara kwa mara,” alisema

“Ukifika Shifaa utashauriwa kipimo sahihi cha kupima ili upatiwe suluhisho la tatizo lako ndiyo sababu mwezi huu tumetoa punguzo kwa uchunguzi wa maradhi ya moyo kwa vijana wanaoanzia miaka 25 hadi 40,” alisema