Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Arusha
Watumishi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), wameiomba Bodi ya Wakurugenzi ya Mfuko huo kuzungumza na Wizara ya Afya juu ya uhuishaji wa miongozo mbalimbali ya huduma za matibabu inayotolewa ili itekelezwe kwa usawa na watoa huduma wote, kwa lengo la kuondoa mkanganyiko unaosababisha baadhi ya wanachama kukosa huduma katika vituo vya kutolea huduma.
Ombi hilo limetolewa jana Aprili 14, 2026 na Watumishi wa NHIF Mkoa wa Arusha wakati wakizungumza na Bodi ya Mfuko iliyokuwa ziarani kukagua utekelezaji wa shughuli za Mfuko kwa ngazi ya Mkoa.
Akiwasilisha ombi hilo, Mkuu wa Idara ya Udhibiti Ubora Dkt. Elika Issowe lisema kuwa, kumekuwepo na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika utekelezaji wa miongozo ya utoaji huduma, hususan ule wa Basic Standards for Health Services (BSHS) uliotolewa mwaka jana, unaobainisha mgawanyo wa huduma katika vituo vya afya kulingana na ngazi na utaalamu wa watoa huduma.
Kwa mujibu wa mwongozo huo, vituo vinavyotambulika kama specialized polyclinics vinapaswa kuwa na madaktari bingwa pekee wanaotoa huduma za kibingwa, huku general polyclinics zikitakiwa kuwa na madaktari wa kawaida (GPs) wanaotoa huduma za msingi.
Alisema kuwa kutokana na mwongozo huu, baadhi ya vituo vya afya vimeanza kufanya mabadiliko ya miundombinu na hadhi ili kuendana na matakwa ya mwongozo huo, hali ambayo imeibua changamoto mpya kwa wanachama wa NHIF.
Kutokana na hali hii, Dkt. Issowe aliiomba Bodi kuangalia uwezekano wa kuishauri Wizara ili kuangalia na kuboresha miongozo hii kwa lengo la kuondoa usumbufu kwa wanachama wanaonyimwa huduma katika baadhi ya Vituo.
“Kwenye baadhi ya vituo, wanachama wa NHIF wamekuwa wakinyimwa huduma au kucheleweshwa kupatiwa matibabu, huku wateja wanaolipa fedha taslim wakipata huduma kwa urahisi zaidi bila vikwazo.Hali hii imeibua malalamiko kutoka kwa wanachama, wakilalamikia kutokuwepo kwa usawa katika utoaji wa huduma licha ya wao kuchangia bima kwa lengo la kupata matibabu bila usumbufu hivyo tunaomba suala hili liangaliwe,” alisema Dkt. Issowe.
Naye Meneja NHIF Mkoa wa Arusha Bw. Hipoliti Lello akiwasilisha taarifa ya utekelezaji kwa Bodi alisema kuwa ubora wa huduma kwa wanachama umeendelea kuzingatiwa ili kuhakikisha wanapata huduma kwa heshima na kwa wakati sahihi.
“Timu yetu ya Udhibiti Ubora imeendelea kufanya kaguzi mbalimbali vituo kwa lengo la kuhakikisha huduma wanazopewa wanachama ni bora lakini pia Ofisi imeendelea na mikakati ya uelimishaji ili kuwafikia na kuwasajili wananchi wengi zaidi,” alisema Bw. Lello.
Bodi ikiongozwa na Mwenyekiti wake Bw. Eliud Sanga aliyeambatana na Prof. George Luhago na Mkurugenzi Mkuu Dkt. Irene Isaka kwa pamoja waliwapongeza watumishi na kuwataka waendelee kufanya kazi kwa bidi na ubunifu mkubwa ili lengo la Serikali la kila Mwannchi kuwa na bima ya afya linafanikiwa.
Bw. Sanga aliwaasa Watumishi kuimarisha mahusiano baina yao mahali pa kazi na nje ya wakati wa kazi ili kujenga ushirikiano na upendo katika kipindi chote watakachokuwa kazini.









