Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Jaffar Haniu, amefanya ziara katika chanzo cha maji Mbaka-Ikama kilichopo kata ya Itagata Barabara ya Katumba -Mwakaleli.

Akiwa katika chanzo hicho Haniu ameuagiza uongozi wa Mamlaka ya Maji Tukuyu Mjini (TUWASA) kuharakisha upanuzi wa chanzo hicho ili kutoa fursa ya kuhudumia zaidi ya wakazi 6,330 waishio Tukuyu Mjini.

”Mheshimiwa rais ametoa fedha nyingi sana kwa ajili ya upanuzi wa chanzo hiki zaidi ya shilingi Billion 3.4 zimetolewa hivyo niwaagize mfanye kazi kwa bidii na weledi ili tuwasogezee hii huduma muhimu katika maeneo yao” ameagiza Haniu.

Mradi huu ulionza kusanifiwa mwaka 2021 unatarajia kuzalisha zaidi ya Lita 45,000 kwa siku huku mahitaji yakiwa ni Lita 22,000 ifikapo mwaka 2042 kwa siku na hivyo kutoa ziada ya maji katika mji wa Tukuyu.

Mradi huu unatarajia kukamilika Mwezi julai 2023 ambapo shughuli za ujenzi zimefikia asilimia 80 zikihusisha ulazaji wa Bomba kuu la mserereko kwa umbali wa Km 9.5 kutoka kwenye chanzo Cha maji hadi kwenye soko la ndizi Msasani ambapo tenki kuu la kupokelea na kuhifadhi maji linatarajia kujengwa, ujenzi wa tenki la kupunguza mgandamizo wa maji, ujenzi wa tenki kuu la kuhifadhia maji eneo la sokoni lenye ujazo wa Lita million 1.5 ambapo ujenzi wake upo asilimia 5 na uchimbaji wa mtaro na kulaza mabomba ya kusambazia maji umbali wa kilometa 20.

Akiwa katika eneo la ujenzi wa tenki katika soko la ndizi Msasani Haniu amemwagiza mkandarasi anayetekeleza Mradi huo kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha kwa wakati kazi hiyo na kuleta tija na Maendeleo kwa Wananchi.

Wakazi wa mji wa Tukuyu kwa Sasa hupata maji kutoka chanzo Cha maji Mlagala, Maswisa, na Msalala ambavyo kwa siku hutoa kiasi Cha Lita za maji 5,880 kwa siku ukilinganisha na mahitaji ya Lita 15,000 kwa siku sawa na asilimia 39.2% ya mahitaji.

By Jamhuri