‘Dk. Magufuli fanya haya tanzanite isiende Kenya’

Tanzanite(5)Haya ni maajabu ya dunia! Licha ya nchi ya Kenya kutokuwa na chembe ya shimo la tanzanite, ndiyo inayojulikana kuwa msafirishaji mkuu wa madini hayo duniani ikifuatiwa na India na Afrika Kusini.

Haya yametokea si kwa bahati mbaya, isipokuwa ni kwa sera na ukosefu wa mbinu za kizalendo za Watanzania ambao kimsingi walipaswa wahakikishe kuwa Tanzania inaendelea kujulikana kuwa ndiyo mzalishaji pekee wa tanzanite duniani.

Hata hivyo, kati ya nchi zinazouza nje madini hayo, Tanzania inashikilia nafasi ya mwisho. Katika soko la dunia mauzo ya tanzanite mwaka 2005 yalikuwa na thamani ya dola milioni 400 za Marekani. Hata hivyo, rekodi ya Tanzania ni dola milioni 16 tu za Marekani.

 Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wa Madini Tanzania (TAMIDA), Sammy Mollel, anasema Serikali ya Awamu ya Tano inapaswa kukomesha ‘dharau’ hii ili madini ya tanzanite yawanufaishe Watanzania kimapato na kisifa kama mzalishaji pekee wa madini hayo ulimwenguni.

Katika mazungumzo na Gazeti hili, Mollel anasema: “Rais ajaye afanye mabadiliko ili Tanzania isiondoke katika ramani ya dunia kibiashara. Kuona kuwa Kenya ndiyo wasafirishaji wakuu wa tanzanite ni aibu, aibu, aibu. Hili sharti liangaliwe na likomeshwe.”

Anayataja mambo kadhaa ili kuondoana na kadhia hii. “Kwanza, Kenya hawana VAT (Kodi ya Ongezeko la Thamani) kwenye madini. Hawana VAT kati ya dealer (muuzaji) na dealer. Hawana urasimu.

Tanzanite inatoroshewa Kenya kwa sababu pia leseni ya muuza madini ni dola 100. Kenya ukishakuwa na leseni hakuna kodi nyingine, isipokuwa corporate tax tu na ya mrahaba ambayo kidogo sana tena wakiwa wameianzisha karibuni. Ukiwa na hivyo tu Kenya unafanya biashara ya madini.

“Wenyewe wanawaza kununua madini yetu kwa thamani kubwa kwa sababu kwao hawana kodi wala urasimu. Hawana VAT. Wageni kwenye viwanja vyao vya ndege wanapata refund (marejesho) ya VAT.

“Wameweka vivutio vingi kwa wafanyabiashara, vikiwamo vya kutowabughudhi,” anasema Mollel.

Anataja sababu nyingine ya Kenya kuwa msafirishaji mkuu wa tanzanite na madini mengine kutoka Tanzania kuwa ni uwepo wa ndege nyingi zinazosafirisha madini nje ya nchi hiyo.

“Wana ndege nyingi. Unaweza kufunga mzigo saa 4 asubuhi na saa 5 asubuhi hiyo hiyo ukasafirishwa. Sisi ni tofauti kabisa. Kenya unachagua mzigo wako uende na ndege ipi.

“Lakini kubwa, gharama zao za usafirishaji ziko chini kabisa. Hali hiyo inawafanya hata Watanzania wapende kwenda kusafirishia mizigo yao ya madini Kenya. Ukifunga mzigo Kenya unalipa dola 2 za Marekani kwa kila kilo moja kwenda Jaipul kwa kutumia ndege ya KQ.

“KQ hiyo hiyo unafunga mzigo Tanzania unachajiwa dola 6 za Marekani kwa kilo moja. Tena mzigo hauendi Jaipul moja kwa moja, isipokuwa unakwenda hadi New Delh, na hapo utapandishwa ndege nyingine hadi Jaipul kwa dola moja kwa kila kilo moja.

“Hii maana yake nini? Maana yake Wakenya wanavutia ili mizigo ya madini isafirishwe kutokea kwao Kenya. Wanatukatisha tamaa kusafirishia kwetu kwa kutuwekea gharama kubwa za usafirishaji. Wanafanya hivyo kwa sababu hatuna ndege zetu. Hiyo imetuletea matatizo, na huo ni ukweli usiopingika,” anasema.

Anasema pamoja na ukweli huo, bado mfanyabiashara akifika Kenya hupokewa kwa heshima na wakati mwingine kwa unyenyekevu.

“Unapokewa kwa kuogopwa, unanyenyekewa. Sisi wenyewe tumeua uchumi wa nchi yetu. Tumejiwekea sheria za kutumaliza, tunataka mabadiliko ili Rais ajaye ayaondoe haya mambo,” anasema.

Kwa ufupi anachosema Mollel ni kwamba ili Kenya isitambulike kuwa msafirishaji mkuu wa tanzanite, Serikali ijayo haina budi kupunguza mlolongo wa kodi kwenye biashara ya madini, kuhakikisha tunafufua shirika letu la ndege la Taifa, urasimu unaondolewa na kufanya mambo kidigitali.

 

CHANGAMOTO NYINGINE

 Mollela anasema Sheria ya Madini ya mwaka 2014 iliyofanya marekebisho kwenye VAT ni changamoto kubwa ambayo Serikali ya Awamu ya Tano isipoirekebisha, biashara ya madini nchini itakufa.

“Sheria hii inahudu refund (marejesho ya VAT). Ilitungwa bila sisi wadau kushirikishwa. Iko hivi, mtalii anapokuwa nchini, akinunua madini huwa kuna VAT. Inabidi akienda uwanja wa ndege wakati wa kusafiri, arejeshewe VAT yake. Sasa utaratibu huo umeondolewa kupitia sheria ya mwaka 2014.

“Hili ni pigo kubwa sana. Wageni wanapokuja kununua madini yakiwa na VAT usipowarudishia hiyo asilimia 18 ya VAT unafanya wasirudi tena.

“Ukienda Bangkok unakaribishwa na bango la ‘NO DUTY, NO VAT. Wenzetu wamefanya vizuri kwa kuondoa yale yanayodumaza biashara ya madini. Madini yote ya Afrika yanapelekwa pale. Wanapata faida kubwa, wanajenga barabara flyover na kadhalika.

“Sheria ya VAT ni kwa mnunuzi wa nyumbani, ukimtoza mgeni  halafu usimrudishie ni dhuluma na atakwenda kututangaza vibaya mwishowe tutakosa wageni na wafanyabiashara.

“Usipomridishia VAT maana yake madini ya Tanzania yanakuwa ghali. Kama hivyo ndivyo, kwanini anunue hapa badala ya kwenda kununua Bangkok?” Anahoji.

Mollel anataja athari za sheria hiyo ya VAT ya mwaka 2014 kuwa ni ongezeko la magendo.

“Watu watalazimika kutorosha madini, Serikali inakosa mapato mengi kwa kudhani VAT itasaidia kumbe ndiyo inayoharibu, hasa hii ya kuto-refund wageni wanaoondaka nchini,” anasema.

Athari ya pili kwa mujibu wa Mwenyekiti Mollel, ni kwamba Maonyesho ya Vito pamoja na Usonara yanayofanyika katika Hotel ya Meru jijini Arusha kila mwaka, yatakufa.

“Haya maonyesha tayari yalishaanza kuwavuta wageni wengi, lakini sheria hii ya kuwafanya wasirudishiwe VAT pale uwanja wa ndege inaua kabisa haya maonyesho. Kama marejesho ya asilimia 18 ya VAT hayatafanywa, maonyesho yatakufa,” anasema.

Anaongeza kuwa Sera ya Madini ya mwaka 2009 imeeleza bayana kuwa madini yakatwe hapa hapa nchini ili yaongezwe thamani.

“Serikali imetamka kuwa itarekebisha na kuboresha kodi na ushuru mbalimbali. Ukiweka hii tozo huko si kuboresha, bali ni kwenda kinyume cha Sera ya mwaka 2009.

“Sera imetamka bayana kuwa kwa muda mfupi Tanzania iwe kitovu cha vito katika Bara la Afrika. Ukitaka Sera hii itekelezwe inapingana na Sera ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha vito Afrika,” anasema.

Mwenyekiti anasema kwa Sera hiyo, ilikuwa madini mengi yaletwe Tanzania kwa ajili ya kuongezewa thamani na kupelekwa nje, lakini hali ilivyo ni kwamba suala hilo halitawezekana.

“Haya mambo ni mazito. Yatazamwe na kurekebishwa na Serikali ya Awamu ya Tano mapema iwezekanavyo ili Maonyesho ya Vito Arusha yasife,” anasema.

Tatizo jingine linalozungumzwa na Mollel ni kukosekana kwa uratibu wa mambo kati ya wizara moja na wizara nyingine.

“Hakuna coordination ya wizara na wizara. Wizara ya Madini inatoa Sera, Wizara ya Madini wanatoa Sheria vinavyokinzana. Huwezi kutoa sera ya kuboresha halafu wizara nyingine ikatoa sera ya kukandamiza,” anasema.

Aprili 19, mwaka huu kutakuwapo maonyesho ya vito jijini Arusha, lakini hofu ya Mollel ni kwamba kwa mgongano wa sera na sheria, hasa ile ya marejesho ya asilimia 18 ya VAT, maonyesho hayo huenda yakakwama.

“Ujumbe ulioenda kwenye Maonyesho ya Madini ya 56 kule Bangkok Septemba 10-14, mwaka huu uliwaambia washiriki wengi waje kwenye maonyesho yetu ya mwakani, lakini kwa mambo yalivyo inawezekana hawatakuja kwa sababu sheria zetu hasa hii ya marejesho ya VAT ni mbaya. Tunapaswa kuinusuru hali hii kwa kurekebisha sheria ili wageni waje.

“Wakijua tuna obstacles (vikwazo) hawatakuja. Yatakuwa maonyesho ya kimataifa yasiyo na wageni. Tuangalie sheria tunazotunga zinaendana vipi na hali ya biashara duniani. It’s a very serious concern (huu ni wasiwasi mkubwa),” anasema Mollel.

Kuhusu changamoto nyingine, anasema zipo, lakini kubwa ni hilo la marejesho ya VAT kwa wageni wanaonunua madini nchini.

“Hili ndilo gumu sana ukiweka na hilo la kwanini Kenya ndiyo wanaoonekana kuwa wasafirishaji wakuu wa tanzanite. Haya mengine ni ya kawaida na yanashughulikiwa na ofisi ya Ofisi ya Kamishna wa Madini. Suala kubwa nasisitiza kuwa ni hii VAT kwa wageni, lazima tuhakikishe inaondolewa ili kupunguza malalamiko, kuimarisha biashara na kuzuia utoroshaji madini nje ya nchi.

“Thailand ni nchi iliyo dunia ya tatu kama sisi, lakini wameweza kufanya mambo makubwa kwenye madini na yamewapa maendeleo kweli kweli. Naamini Awamu ya Tano itaifanya Tanzania iipiku Thailand,” anasema Mollel.