Msanii wa Singeli, Dulla Makabila ametakiwa kufika Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ili kujadili wimbo wake mpya uitwao ‘Pita Huku’ ambao kwa sasa unafanya vizuri kwa kuwa na watazamaji wengi katika mtandao wa YouTube.

Makabila amepata barua wito huo kutoka kwa Katibu Mtendaji, Dkt. Kecnon Mapana ambayo imesomeka kwamba “BASATA Inapenda kuwajulisha kwamba kutakuwa na kikao kitakachofanyika tarehe 21/12/2022 siku ya Jumatano, ajenda ya kikao ni kujadili kuhusiana na wimbo wako wa Pita Huku.”

Msanii huyo amekubali wito huo kupitia ukurasa wake wa Instagram ambapo ameandika kuwa,

“nimepokea barua ya wito kutoka BASATA ambayo inahusu wimbo wangu mpya, wito nimeupokea na nitafika leo BASATA, nyie ni walezi wangu katika shughuli zangu za Sanaa. naimani utakua wito wa kheri.”

“Mashabiki zangu asanteni Kwa kuufanya wimbo wetu wa Pita Huku’ kuwa trending number moja huko mjini Youtube, tuendelee kufuatilia kazi nzuri.”