Teknolojia ya Habari na Mawasiliano yakiwamo matumizi na mitandao ya kijamii
yamewezesha wepesi na ukaribu wa mawasiliano ya watu duniani kiasi cha
kuthibitisha ukweli wa ‘Dunia Kiganjani’ au ‘Dunia kama kijiji kimoja.’ 

Pamoja na manufaa haya bado ukweli ulio dhahiri ni kuwa matumizi ndiyo yanayoamua
heri na shari, faida na hasara, wema na ubaya, elimu na ujinga na hata uhalifu wa
watumiaji wa mitandao hiyo.
Idili ya makala hii ni kutoa angalizo na nasaha juu ya matumizi mabaya ya
mitandao ya kijamii na hususan malumbano yasiyo na staha baina ya Wakristo na
Waislamu mitandaoni.
Katika Facebook, kwa mfano, kuna mtandao unaoitwa ‘UISLAMU VS
UKRISTO NI IPI NJIA YA KWELI?” ambao unahusisha mamia ya washiriki na
ukifuatilia malumbano yanayoendelea na ushabiki wa kidini unaokuzwa na
makundi ya wana dini hizi pamoja na kauli chafu na kebehi zinazotumiwa, utabaini
kuwa hazina afya njema kwa uhusiano wa Waislamu na Wakristo nchini kwetu.
Linalosikitisha sana ni kuwa sumu hii inaenezwa na watu wasio na ujuzi wa dini; si
taaluma ya Uislamu wala theolojia ya Ukristo. Tuwasaidie kidogo.
Kwanza kabisa, walipaswa kufahamu nini Ukristo na nini Uislamu. Bila ya
kuzama kwenye fasili za mabingwa wa Theolojia na Historia za Dini, kwa mujibu
wa Kamusi Elezo Huru, Ukristo (kutoka neno la Kigiriki Khristos, ambalo linatafsiri
lile la Kiebrania  Māšîăḥ, linalomaanisha ‘Mpakwa mafuta’.
Ni  dini  inayomwamini  Mungu  pekee kama alivyofunuliwa
kwa  Waisraeli  katika  historia ya wokovu  ya  Agano la Kale, hasa Yesu Kristo
(Amani iwe juu yake) katika Agano Jipya ambaye ni  mwanzilishi wake katika karne
ya 1 . 

Kamusi Elezo Huru pia imeueleza Uislamu (kwa Kiarabu Al-Islam) kuwa
ni  dini  inayotokana na mafunzo ya  Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na
Ampe Amani). 

Uislamu ni ile imani kuwa  Muumba  ni Mmoja tu kwa dhati na sifa
zake.  Nguzo nyingine za imani zinajengwa juu ya imani ya Mungu Mmoja wa
kweli, imani juu ya maisha baada ya kifo, imani juu ya Malaika wa
Mungu, vitabu vyake na kudra na tafsiri ya vitendo ya imani hii
ni:  Sala, Zakah, Saumu na Hija.
Fasili hii ya Uislamu ni finyu na inauzungumzia Uislamu ukihusishwa na Mtume
Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani). Ama Uislamu kwa tafsiri pana
ni Dini ya Allaah waliyokuja nayo mitume wote tangu Adam (Amani iwe juu yake)
hadi Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) na huo ni mfumo
kamili na muongozo wa maisha ambao Mwenyeezi Mungu amewatuma mitume
wake (Amani iwe juu yao) waufikishe kwa watu ili waufuate katika vipengele
vyote vya maisha yao.
Dini mbili hizi ambazo msingi wake mkuu, kwa mujibu wa fasili iliyotangulia, ni
Imani ya Mungu Mmoja Pekee ni miongoni mwa dini tatu zinazohusishwa na
Mtume Ibrahimu (Amani iwe juu yake) hivyo kuitwa Dini za Ibrahimiya. Dini ya
tatu ni Uyahudi.
Katika makala hii ninakusudia kuyaweka wazi baadhi ya mambo mawili
yanayozihusu dini mbili hizi za Uislamu na Ukristo ambazo ndizo dini kuu nchini
Tanzania ili mambo haya yaturejeshe katika mstari wa tafakuri sahihi ya uhusiano
wa dini mbili hizi nje ya yale yaliyozikumba kama athari hasi za ukoloni
mkongwe, ukoloni mamboleo, mila na desturi za watawala waliotumia dini kama
nyenzo ya kutawalia, propaganda za kuutukuza Uarabu (Arabization) na Uzungu
wa Mashariki na Magharibi (Eastern and Western Civilization).
Nimetangulia kueleza kuwa Ukristo na Uislamu (kwa tafsiri finyu) ni dini
zinazohusishwa na Mtume Ibrahimu (Amani iwe juu yake) kwa kuwa ni dini
zinazohusishwa na ufunuo uliofikishwa kwa manabii na mitume kupitia Malaika
Jibril. Dini hizi zinaitwa dini za mbinguni na zote zinaamini Siku ya Hukumu na
kulipwa Pepo au kuadhibiwa motoni.
Kuna umuhimu mkubwa kwa hawa wanaolumbana na kukashifiana kuhusu
Uislamu na Ukristo mitandaoni na popote pale wayajue haya yafuatayo:
1. Uislamu uliutambua Ukristo wa Roma.
Wakati nafuatilia mafunzo ya Shahada yangu ya Kwanza iliyokusanya Falsafa,
Taaluma za Dini na Lugha ya Kiswahili nilikumbana na wasomi wanaouhusisha
Ukristo na Wayahudi na kwamba wanaposoma kwenye Qur’aan Tukufu habari za
Wakristo huamini Ukristo unaozungumziwa ni ule unaowahusu Wayahudi. Ukweli
ni kuwa Wayahudi hawajapata kuwa Wakristo kwani kwao Uyahudi ni dini,
kabila na taifa.
Tunaposoma katika Qur’aan Tukufu tunaikuta Sura ya 30 (Surat Ar-Rum). Neno
Ar-Rum lina maana ya ‘Roma’. Sura hii inalielezea tukio lilitokea mwaka 613
ambapo Waajemi (Washirikina wanaoabudu moto) waliwashinda Warumi
(Wakristo, Watu wa Kitabu). 

Habari hii ilipowafikia Washirikina (wanaoabudu
masanamu) wa Makkah walifurahi sana na walimwambia Mtume Muhammad
(Allaah Amrehemu na Ampe Amani) kuwa: “Wakristo (Warumi), watu wa Kitabu
kama nyinyi, wameshindwa na washirikina wenzetu, na hii ni alama ya kuwa
karibuni na sisi tutakushindeni.”
Qur’aan Tukufu ikajibu tambo hizo kwa kutoa bishara mbili zitakazotokea wakati
mmoja nazo; mosi, Wakristo Warumi kuwashinda Waajemi Washirikina, na pili,
Waislamu kuwashinda Washirikina wa Makkah. Tunasoma katika Qur’aan Tukufu
Sura ya 30 (Surat Ar-Rum) Aya ya 2 hadi ya 6 kuwa:
“Warumi wameshindwa. Katika nchi iliyo karibu (na nchi ya Bara Arabu. Nayo ni
Shamu), nao baada ya kushindwa kwao, watashinda. Katika miaka michache, Amri
ni ya Mwenyeezi Mungu kabla (yake) na baada (yake); na siku hiyo (Warumi
watakaposhinda) Waislamu watafurahi. Kwa nusura ya Mwenyeezi Mungu
(Anayowapa wao. Nayo ni kuwashinda Washirikina wa Makkah siku hiyo).
(Mwenyeezi Mungu Humnusuru Amtakaye, naye ni Mwenye nguvu (na) Mwenye
rehema. (Hii ni) ahadi ya Mwenyeezi Mungu, Mwenyeezi Mungu havunji ahadi
yake, lakini watu wengi hawajui.”
Naam. Bishara hii njema ilitimia kwa Hirakla, Mfalme wa Warumi, kuingia Media
(Madayin) katika nchi ya Waajemi na mwaka huohuo Waislamu 313 walilishinda
jeshi la Washirikina wa Makkah lenye watu 1,000 mastadi wa vita waliokuja kwa
nia ya kuwaangamiza Waislamu. Vita vikapiganwa katika Mtaa wa Badri na
Washirikina wakashindwa vibaya.
Tunachojifunza hapa ni kuwa wakati Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na
Ampe Amani) anapewa Utume mwaka 610 A.D. Ukristo alioukuta ni Ukristo wa
Roma (Ukatoliki) ambao ulishaenea hapo tangu mwaka 313 A.D.
Wakati  Kaisari Konstantino Mkuu  alipotangaza huko Milano uhuru wa dini  kwa
wananchi wote na ukashamiri mwaka 380 wakati Kaisari Theodosius wa
Kwanza, alipoufanya Ukristo wa Kikatoliki kuwa dini rasmi ya Dola ya Kirumi.
2. Padri wa Kikatoliki alimuokoa Mtume Muhammad asiuawe.
Katika Historia ya maisha ya utotoni ya Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na
Ampe Amani) tunasoma tukio lilitokea mwaka 582 A.D. ambapo Mtume
Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) akiwa na umri wa miaka 12
alifuatana na baba yake mdogo, Abu Twalib Bin Abdil-Mutwalib, kwenda Shamu,
lakini walipofika  Busra  – mji wa kusini kabisa katika nchi ya Shamu – walikutana
na padri jina lake Bahira ambaye alimkataza asisogee na mwanawe zaidi kuliko
hapo, akamwambia: “Mtoto huyu namwona ana alama zote za Mtume
aliyetabiriwa kuwa atakuja, basi naona ni hatari kubwa akienda Shamu, asije
akauawa na Wayahudi huko. Nakusihi sana urejee naye, au umpe mtu mwaminifu
arejee naye, nawe uende katika biashara zako”. Abu Twalib alimpa mtu arejee
naye Makka naye akaendelea na safari yake.
Kitendo cha padri huyu kumnusuru Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na
Ampe Amani) na shari za Wayahudi ambao kwa elimu waliyonayo, kama
aliyokuwa nayo padri huyu, wangeng’amua alama za utume alizokuwa nazo
Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) na wangeamua kumuua,
kinasadifu yaliyokuja kwenye Qur’aan Tukufu juu uhusiano wa watu wa dini hizi
tatu za Ibrahimiyya – Uyahudi, Ukristo na Uislamu.
Tunasoma katika Qur’aan Tukufu, Sura ya 5 (Surat Al-Maidah) Aya ya 82 kuwa:
“Hakika utawakuta walio shadidi kuliko watu wote katika uadui kwa
walioamini (Waislamu) ni Mayahudi na Washirikina. Na utawakuta walio karibu
mno kwa mapenzi ni wale wanaosema: Sisi ni Wakristo. Hayo ni kwa sababu
wapo miongoni mwao makasisi (mapadri) na watawa (wamonaki), na kwa sababu
wao hawafanyi kiburi.
Katika tukio hili na mafunzo haya ya Qur’aan Tukufu tunajifunza uhusiano
mwema, kuhurumiana na mapenzi mema yaliyokuwapo na yanayostahili
kuendelea kuwapo baina ya Waislamu ambao wametakiwa kujipamba na uadilifu
na kutenda haki na insafu kwa wote na Wakristo wenye mapenzi kwa watu
wakiwamo Waislamu na ambao wanapambwa na tabia njema zinazoongozwa na
makasisi na watawa wasio na kiburi.
Kama hali ni hii, kwa nini tunawapa nafasi wale wanaopanda chuki kwa misingi ya
kidini katika jamii yetu? 

Wanafanya hayo kwa mafundisho ya nani? Kiburi, kebehi
na maneno yasiyo ya staha yanayotolewa na wanaofanya malumbano mitandaoni
yanafuata mafunzo yepi nje ya mafunzo ya Uislamu na Ukristo wanaokwenda
tofauti nayo?
Nihitimishe makala hii kwa kuwakumbusha Waislamu na Wakristo kurudi katika
mstari wa asili wa uhusiano mwema na mapenzi baina yao, jambo tunalolihitajia
sana katika kuimarisha umoja na mshikamano wa taifa letu la Tanzania ili kujenga
nyenzo muhimu za kupambana na changamoto mbalimbali za kitaifa na kimataifa.
Hatuna budi kuchuja na kupembua mafunzo sahihi ya dini zetu na biashara na
propaganda za wale wanaotumia dini kama nyenzo ya kufanikisha malengo yao
mabaya kwetu na yasiyo na faida nasi. 

Msingi wa dini zote mbili hizi ni kuhubiri amani, upendo, kuhurumiana, kusaidiana na kuishi vema tukiwa ndugu na
majirani. Yeyote anayehubiri kinyume cha haya huyo ana yake na hatutakii mema.
Haya tukutane Jumanne ijayo In-Shaa-Allaah.
Sheikh Khamis Mataka ni Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu
la Waislamu wa Tanzania (Bakwata).
Simu: 0713603050/0754603050

By Jamhuri