Halmashauri ya Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma imepokea zaidi ya shilingi bilioni tatu kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta ya elimu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Neema Maghembe amesema kati ya fedha hizo  Halmashauri imepokea fedha zaidi ya shilingi milioni 149 kupitia Ufadhili wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (Tanzania Education Authority- TEA) kwaajili ya ujenzi wa bweni la wasichana lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 120.

Amesema Halmashauri hiyopia imepokea fedha kiasi cha shilingi milioni 362.2 kutoka katika kampuni ya Barrick Gold Mine Tanzania kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu katika shule ya sekondari Maposeni.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Songea Neema Maghembe akishiriki kusambaza udongo kwenye mradi wa ujenzi wa vyoo katika shule ya sekondari Maposeni

Maghembe amesema fedha hizo zitatumika kujenga madarasa manne ambapo kila darasa litagharimu shilingi milioni 24.

Ameongeza kuwa fedha hizo pia zitajenga mabweni mawili ambapo kila bweni litagharimu shilingi milioni 128  na ujenzi wa matundu ya vyoo sita ambapo kila tundu litagharimu kiasi cha shilingi milioni 1.7.

“Kampuni ya Barrack imetoa fedha hizo ili kuunga mkono jitihada na juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuboresha elimu nchini’’,alisema.

Hata hivyo amelitaja lengo la ujenzi wa miundombinu hiyo kuwa ni kuwezesha wanafunzi waliofaulu kujiunga na kidato cha tano mwaka 2023, kupata fursa ya kuendelea na masomo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Neema Maghembe

Kulingana na Mkurugenzi huyo,Halmashauri  hiyo pia imepokea fedha kiasi cha shilingi milioni 834 kutoka Serikali kuu kwa ajili ya kuongeza miundombinu ya wanafunzi wa kidato cha tano katika shule ya sekondari Jenista Mhagama.

Amesema  fedha hizo zitatumika kujenga madarasa 12 ambapo kila darasa litagharimu fedha kiasi cha shilingi milioni 24,mabweni manne ambapo kila bweni litatumia  kiasi cha shilingi milioni 128 na ujenzi wa matundu ya vyoo 20 ambapo tundu moja litagharimu shilingi milioni 1.7.

Amesema Halmashauri hiyo pia imepokea fedha kiasi cha shilingi milioni 751.8 kutoka Serikali kuu kaajili ya kuongeza miundombinu ya wanafunzi wa kidato  cha tano katika shule ya sekondari Mpitimbi.

Amesema fedha hizo zitatumika kujenga madarasa tisa ambapo kila darasa litagharimu shilingi milioni 24,ujenzi wa mabweni manne ambapo kila bweni litagharimu shilingi milioni 128 na ujenzi wa matundu ya vyoo 14 ambapo tundu moja litagharimu milioni 1.7.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa  Halmashauri  ya Wilaya ya Songea Mheshimiwa Menas Komba  ameishukuru Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mbunge wa Jimbo la Peramiho Mhe. Jenista Joakim Mhagama kwa kuendelea kuimarisha miundombinu ya elimu.

Imeandikwa na Albano Midelo,Ruvuma