Na Dennis Luambano, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Ubalozi wa Japan nchini Tanzania umetoa ruzuku ya ufadhili wa miradi miwili katika manispaa za Tabora na Ubungo.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini mikataba ya miradi hiyo iliyofanyika Dar es Salaam Oktoba 27, 2026, Balozi wa Japan hapa nchini, Mikami Yoichi, ameutaja mradi wa kwanza ni ufungaji wa vifaa tiba kwa ajili ya huduma za matunzo ya watoto wachanga na mjamzito hadi atakapojifungua katika wodi tatu za Manispaa ya Tabora mkoani Tabora wenye ruzuku ya Dola 111,758 za Marekani.

Amesema mradi huo utatoa vifaa tiba muhimu kwa vituo vitatu vya afya na kusaidia kutoa huduma za kujifungua kuwa salama zaidi kwa akina mama 1,000 na watoto wao wachanga.

“Miradi hii miwili ina lengo la pamoja la kuwasaidia akina mama, watoto wachanga na familia kupata huduma bora za afya na kuishi maisha yenye afya zaidi. Lengo hili linaendana na Dira ya Maendeleo 2050 ya Tanzania [Dira 2050] inayolenga kufikia huduma za afya kwa wote na kukomesha vifo vya akina mama, watoto wachanga na watoto.

“Kwa miaka iliyopita, Japan imefadhili miradi kadhaa ya maendeleo katika ngazi ya jamii mkoani Tabora. Mwaka 2010, Ubalozi wa Japan uliunga mkono upanuzi wa zahanati katika Wilaya ya Uyui.

Tunafurahi kushirikiana tena na Jimbo Kuu la Kanisa Katoliki la Tabora ambaye ni mshirika wetu tunayemthamini, amesema.

Ameutaja mradi wa pili kuwa ni ujenzi wa Zahanati ya Gogoni katika Manispaa ya Ubungo, Dar es Salaam wenye ruzuku ya Dola 119,477 za Marekani.

Kupitia ruzuku hiyo, amesema watajenga jengo la huduma za wagonjwa wa nje, wodi ya wazazi, vyoo na miundombinu ya maji na kutoa vifaa tiba.

Amesema mradi huo utawanufaisha takribani watu 120,000 katika eneo la Kibamba na maeneo yanayolizunguka na utasaidia kuboresha upatikanaji wa huduma muhimu za afya kwa jamii za Manispaa ya Ubungo.

Kwa Dar es Salaam, amesema hadi sasa Japan imefadhili jumla ya miradi 17 ya maendeleo katika ngazi ya jamii na miradi 391 kote Tanzania yenye thamani ya jumla ya Dola milioni 28 za Marekani tangu mwaka 1989.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kibamba, Angellah Kairuki, amesema kwa kushirikiana na Manispaa ya Ubungo na serikali watahakikisha zanahati hiyo ina wafanyakazi na vifaa tiba kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa kwa miaka mingi ijayo.

Naomba niahidi kwamba kama mbunge nitafuatilia utekelezaji wa mradi huu kuanzia tofali la kwanza litakapoanza kujengwa hadi mgonjwa wa kwanza atakapoanza kutibiwa.

“Tutakuwa na uaminifu kwa kuhakikisha ruzuku hiyo inatumika kwa uwazi, uwajibikaji na thamani ya fedha inaonekana kama masharti ya mkataba huu yanavyotaka, amesema Angella ambaye pia ni Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Pia amesema kwa familia nyingi zinazoishi Gogoni ujenzi wa zahanati hiyo ni muhimu kwa sababu kwa sasa huduma za afya wanazifuata umbali wa kilometa 15.

Wakati wa msimu wa mvua umbali huo unakuwa mkubwa zaidi kwa sababu ya ubovu wa barabara. Fikiria mjamzito anayepata uchungu wa kujifungua usiku wa manane, mfikirie mtoto anayepata homa au mfikirie mzee anayehitaji dawa.

Kwao umbali si kilometa za ramani bali ni huduma wanazozipata kwa wakati au kwa kuchelewa? Kwa watu wa Gogoni, zahanati hiyo ni yenu kwa hiyo itunzeni, muithamini na kuilinda, amesema.

Naye Meya wa Ubungo, Lawrence Mlaki, amesema Gogoni ni miongoni mwa maeneo huduma za afya ya msingi zinahitaji kuimarishwa ili kukidhi mahitaji ya wanaoishi eneo hilo na jamii inayolizunguka.

Amesema ujenzi wa Zahanati ya Gogoni ni hatua muhimu ya kusogeza huduma za afya karibu na wananchi ili kupunguza muda na gharama za safari, kuboresha upatikanaji wa huduma za kinga, matibabu, afya ya uzazi na afya ya mtoto.

Kupitia zahanati hiyo, amesema wanatarajia kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya ya msingi zikiwamo za kliniki ya wajawazito, kujifungua salama kulingana na uwezo wa kituo, huduma baada ya kujifungua, huduma za afya ya watoto wachanga na watoto wenye umri chini ya miaka mitano, chanjo, uzazi wa mpango, uchunguzi wa magonjwa, matibabu ya awali, huduma za kinga na elimu ya afya.

Uwapo wa kituo hiki utasaidia kupunguza rufaa zinazoepukika kwa kuboresha upatikanaji wa huduma zinazotolewa katika ngazi ya zahanati, huku wagonjwa wanaohitaji huduma za kibingwa wakipewa rufaa kwenda vituo vinavyotoa huduma hizo, amesema.

“Msaada huu una thamani kubwa kwa wananchi wa Gogoni kwa sababu unashughulikia moja kwa moja mahitaji yao ya msingi ya huduma za afya. Tunaamini ushirikiano huu utaacha athari chanya ya kudumu kwa jamii unavyoweza kuchangia maendeleo ya huduma za kijamii, amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Tabora, Dk. John Pima, ameshukuru mradi huo unakusudia huduma za matunzo ya watoto wachanga na huduma za kipindi cha kuzaliwa.

“Kuzaliwa kwa mtoto kunapaswa kuwa wakati wa furaha na matumaini kwa kila familia. Hata hivyo, matatizo yanayotokea wakati wa ujauzito, kujifungua na siku za kwanza za maisha yanaweza kuwaweka akina mama na watoto wachanga katika hatari kubwa.

Kwa hiyo, upatikanaji wa vifaa tiba vinavyofaa na huduma bora za afya ni muhimu katika kuokoa maisha na kuwapa watoto mwanzo mzuri wa maisha, amesema.

Kupitia mradi huo, amesema watu wanaopata huduma za matibabu katika Hospitali ya Misheni ya St. Ann, AMUCTA na Zahanati ya Kipalapala watanufaika na upatikanaji bora wa vifaa muhimu kwa ajili ya huduma za afya ya mama na mtoto mchanga.

Kwa niaba ya Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, amesema anatambua mchango muhimu wa Jimbo Kuu la Kanisa Katoliki la Tabora na vituo vya afya vinavyoshiriki katika kufanikisha mradi huo.

“Ushirikiano kati ya serikali, taasisi za afya zinazomilikiwa na taasisi za kidini na washirika wa maendeleo wa kimataifa unaonyesha kile tunachoweza kufanikisha tunapofanya kazi pamoja kuelekea lengo moja.

“Kama Manispaa ya Tabora, tunatambua kwamba kupokea ruzuku hii pia kunaambatana na wajibu. Tumejizatiti kufanya kazi kwa karibu na Jimbo Kuu la Tabora pamoja na vituo vya afya vitakavyonufaika ili kusaidia utekelezaji wenye mafanikio wa mradi huu.

Tutahimiza matumizi sahihi, matengenezo na uwajibikaji katika matumizi ya vifaa hivyo ili kuhakikisha manufaa ya uwekezaji huu yanaendelea kudumu na kuwafikia walengwa, amesema.

Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki Tabora, Josaphat Bududu, amesema ruzuku hiyo itasaidia Hospitali ya Misheni ya St. Ann, AMUCTA na Zahanati ya Kipalapala zinazomilikiwa na Kanisa Katoliki na watawahudumia wagonjwa bila upendeleo.

“Jimbo Kuu lilitambua hitaji la kuboresha vifaa tiba kupitia tathimini ya vituo hivi na likachukua hatua ya kutafuta msaada kutoka kwa washirika wa maendeleo. Tunashukuru Serikali ya Japan ilisikiliza mahitaji yetu na kuitikia kwa ukarimu.

“Mradi huu unahusu zaidi ya vifaa tiba. Unahusu kulinda maisha ya akina mama na watoto wachanga, kuimarisha wataalamu wetu wa afya na kuzipa familia matumaini zaidi wakati wa kujifungua na katika siku za kwanza za maisha ya mtoto, amesema.