Na Abel Paul wa Jeshi la Polisi

Jeshi la Polisi limeipongeza Benki ya NMB kwa namna ambavyo inashiriki katika mapambano dhidi ya uhalifu hapa nchini kwa kutoa elimu na ufadhili wa vipindi katika vyombo vya Habari Tanzania ambapo elimu hiyo imesaidia kuyafikia makundi mbalimbali katika Jamii.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es salaam (DPA) Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Dkt. Lazaro Mambosasa ambapo amebainisha kuwa benki hiyo imekuwa mfano mzuri katika mapambano dhidi ya uhalifu huku akisema kuwa wameitika kutoa Jezi kwa ajili ya mashindano ya Polisi Jamii DPA CUP ambayo yameanza siku ya jana na yatahusisha kata zote za wilaya ya Temeke na chuo hicho.

Ameongeza kuwa lengo la mashindano hayo ni kuwajengea uwezo askari hao walioko mafunzoni namna ya kushirikisha jamii katika mapambano dhidi ya uhalifu hapa nchini.Pia mashindano hayo yanaenda sambamba na utoaji wa damu kwa ajili ya benki ya damu salama ili kusaidia Watanzania wanaopata changamoto ya damu hasa mama wajawazito wanaojifungua na majeruhi wa ajali.

Kwa upande wake Meneja mwandamizi wa wateja maalum kutoka benki ya Nmb Queen Kilnyamagoha amesema wao Nmb wamekuwa na mahusiano ya muda mrefu na Jeshi la Polisi hapa Nchini huku akiweka wazi dhamira yao ya kuendelea na mashirikiano na Jeshi hilo katika mapambano dhidi ya uhalifu.

Nae Afisa Michezo toka chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es salaam (DPA) Mrakibu Mwandamizi wa Polisi SSP Salum Madongo amesema tayari michezo hiyo imeanza siku ya jana huku akibainisha kuwa michezo zaidi ya kumi na sita itachezwa katika mashindano hayo ya Polisi Jamii DPA CUP.