Na Alex Kazenga, Jamhuri Media, Dar es Salaam

Mkutano wa Jukwaa la Mfumo wa Chakula Afrika (AGRF- Africa Food Systems Summit 2023) unaofanyika nchini katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNICC) kuanzia leo, Septemba 5 hadi 8 mwaka huu, utakuza kilimo na kuchochea usalama wa chakula, ustawi wa kiuchumi na uendelevu wa maliasili nchini.


Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus, akiuzungumzia mkutano huu mbele ya wahariri wa vyombo vya habari Ikulu, Dar es Salaam, Septemba 3, mwaka huu, alisema pia utaleta matokeo muhimu kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla.


Matokeo yanayotajarajiwa ni pamoja na kuongezeka kwa uwekezaji katika sekta ya kilimo nchini, kukuza utalii, kuimarika kwa biashara ya mazao ya kilimo na teknolojia, anasema Zuhura.


Mkutano huu wenye wageni zaidi ya 3,000 kutoka mataifa 70 kote duniani, miongoni mwao wakiwamo wakuu wa nchi, watu maarufu, watunga sera, wafanyabiashara wakubwa, wawekezaji, wakulima, vijana, wanawake na wote walioko kwenye mnyororo wa sekta ya kilimo, pia utachochea fursa ya utalii wa kilimo nchini (Agro-tourism).


Anasema hoteli zote pamoja na vivutio vilivyopo Dar es Salaam, Zanzibar na katika maeneo yenye mbuga zinatarajiwa kupata watalii wa kutosha huku sekta ya usafirishaji na ukarimu vikitajwa navyo kupiga hatua.
Wengi mnaweza kujiuliza mifugo na uvuvi vinaingia vipi kwenye mkutano huu wa AGRF, lakini ni wazi tukila chakula ni lazima kuna nyama, kuna samaki, kwa hiyo ndiyo maana Waziri wa Mifugo na Uvuvi na Katibu Mkuu wake nao wanaingia humo, anasema Zuhura.
Aidha, anasema kilimo ndicho kinachopewa kipaumbele katika mkutano huu kutoka na mbadiliko ya kila siku na watu kuongezeka, hivyo wataalamu wamelazimika kutafuta namna ya kukidhi mahitaji ya watu kwenye chakula kote duniani.
Bahati nzuri Tanzania tuna ardhi yenye rutuba, yenye uwezo wa kuzalisha chakula cha kutosha na kingine kuuzwa hadi nje ili kusaidia upatikanaji na usalama wa chakula barani Afrika.
Kwenye mifugo nako si pabaya sana. Kwa mujibu wa takwimu za sasa Tanzania ina ngombe milioni 36.6, mbuzi milioni 26.6, kondoo milioni 9.1 na kuku milioni 97.1.
Tukija kwenye maziwa na mito nako kuna samaki wa kutosha; kwa Ziwa Victoria peke yake Tanzania ina akiba ya samaki kiasi cha tani milioni 2.23, anasema Zuhura.
Katika mkutano huu wa AGRF, Tanzania inakuwa mwenyeji kwa mara ya pili, ambapo mara ya kwanza ilikuwa mwenyeji mwaka 2012, wakati huo Jukwaa likifahamika kama Jukwaa la Mapinduzi ya Kijani Afrika (Africa Green Revolution Forum).
Taarifa za Tanzania kuwa mwenyeji zilitangazwa Desemba 12, mwaka jana, katika mkutano wa biashara uliofanyika Marekani, ukihusisha Marekani na mataifa ya Bara la Afrika (US- Africa leader Summit).
Kichocheo cha kuchaguliwa kuwa mwenyeji kinatajwa kuwa mageuzi makubwa ambayo Serikali ya Awamu ya Sita imeyafikia kwenye kilimo tangu imeingia madarakani.
Mageuzi hayo ni pamoja na kuongeza bajeti kwenye kilimo na kuanzisha mpango kabambe wa BBT (Building Better Tomorrow) unaowalenga mahususi vijana kwenye sekta ya kilimo.
Kwa kifupi mkutano huu unahusu chakula. Tunaweza kuzungumzia mambo chungu nzima, lakini kama haujala mambo hayaendi, kwa hiyo kila mmoja wetu unatuhusu, anasema Zuhura.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, akielezea maendeleo ya wizara yake katika mkutano huo, anasema imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali, yakiwamo maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha vijana na wanawake wanajihusisha pia kwa wingi katika sekta ya mifugo na uvuvi.
Mkutano huu ambao awali uliihusu sekta ya kilimo moja kwa moja, Waziri Ulega anasema kwa kipindi hiki unapofanyika nchini pia umetoa fursa kwenye sekta ya mifugo na uvuvi tofauti na miaka ya nyuma.
“Jitihada za Rais Samia zimesababisha mkutano huu uje Tanzania, hiyo inaonyesha nia ya Rais kuwainua wananchi walio wengi kwenye kilimo – mazao, kilimo – mifugo na kilimo – uvuvi.
Anasema kupitia mkutano huo sekta ya kilimo – mifugo na kilimo – uvuvi zitagusa watu wengi, hivyo kwa maono ya Rais Samia zitaleta tija kwa pamoja.
Akifafanua masoko ya mifugo na nyama, anasema Tanzania imejipanga na kuweka mikakati mbalimbali ya soko la nyama huku akisisitiza kuwapo uhamasishaji kwa wananchi, hasa kuhusu fursa adhimu iliyopo kwenye biashara ya mifugo.
Wahariri wa vyombo vya habari, biashara hii ni fursa kubwa sana, mtusaidie kuelezea biashara hii, uzuri wa unenepeshaji na kuingiza katika viwanda, tuchakate na tuweze kuingiza nje.
Lakini tunahitaji na mitaji iende, kazi yenyewe inahitaji fedha, tuna mitaji ambayo tunailenga ambayo ndiyo dhumuni la mkutano huu wa AGRF. Tuna mitaji ya mabenki yetu ya ndani, tunataka tuwaaminishe waingize fedha huko ili twende tukatengeneze wafugaji walioko kwenye biashara, anasema.
Anasema wafugaji walio wengi hawako kwenye biashara ya kunenepesha mifugo, hivyo kupitia Wizara ya Mifugo wanachohangaika nacho ni kuwachukua wafugaji hao na kutengeneza tabaka la pili ambalo litakuwa muhimu katika kushirikiana na wafugaji wa kawaida kuchagua mifugo ya kununua na kunenepeshwa kwa ajili kupelekwa kwenye masoko yanayohitaji mifugo iliyo nawili.
Ili tupate takaba la pili la wafugaji ni lazima mitaji na teknolojia vipatikane, pamoja na uzoefu, tunaushukuru mkutano huu, wenzetu hapa Afrika na kwingine duniani hizi hatua wamekwisha kuzipiga, anasema Ulega.
Kwa upande mwingine anasema pamoja na mipango hiyo wanao mpango wa kutumia ardhi vizuri, ikiwamo ardhi ya Shirika la NARCO – National Ranching, ambalo anadai kwa muda mrefu halijafanya vema.
Anasema serikali imejipanga vema kutumia ardhi hiyo huku akidai moja ya mkakati wanaokwenda nao ni kuwapeleka vijana wa BBT kama tabaka la pili wanalolitengeneza.
Tunatengeneza wafanyabiashara wa mifugo ambao lengo letu ni kwenda sokoni, hasa kwenye minada kufundishwa namna ya kuchagua ngombe.
Si kila ngombe unayemchukua kwenye mnada atafaa kwenda kunenepesha, hapa tuna wataalamu na wazoefu wanaowafundisha vijana kumtazama ngombe – fremu yake na umri wake. Wanabaini ngombe huyo akipewa chakula kwa siku kadhaa atawapa kile wanachokihitaji, aidha kwa kuongezeka nusu kilo au kilo moja.
Vijana ambao tumewachukua wameanzia sokoni kwenda kununua na wamepata faida nzuri sana. Katika vijana 240 tuliofanikiwa kuanza nao kila mmoja ana ngombe 10 ambao amekwenda kuwachagua na kuwanununua mnadani mwenyewe na kuwanenepesha, anasema Ulega.
Ulega anasema tangu mradi huo umeanza vijana hao tayari wameuza takriban ngombe 900, ambapo wamepata faida ya kuingiza Sh milioni 74 katika akaunti zao za benki.