NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Shirika la Masoko ya Kariakoo limezindua Kituo cha Huduma kwa Wateja kwa lengo la kurahisisha upokeaji na utatuzi wa changamoto za wafanyabiashara, huku watumishi wakitakiwa kuzingatia lugha nzuri, heshima na staha wanapotoa huduma.
Wito huo umetolewa na Katibu Tawala wa Halmashauri ya Wilaya ya Ilala, Charangwa Selemani, leo jijini Dar es Salaam, wakati akizindua kituo hicho kinacholenga kuimarisha mawasiliano kati ya shirika hilo na wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao katika soko hilo.
Charangwa amesema uzinduzi wa kituo hicho utakuwa na manufaa zaidi iwapo utaambatana na huduma bora, uwazi, usalama na utatuzi wa kero za wafanyabiashara kwa wakati.
Amesisitiza kuwa kituo hicho kinapaswa kupatikana saa 24 kwa siku ili kuhakikisha simu za wafanyabiashara zinapokelewa na changamoto zao kushughulikiwa ipasavyo.
Amesema ni muhimu watumishi wa kituo hicho kupewa mafunzo na semina zitakazowawezesha kuwasikiliza na kuwahudumia wateja kwa weledi, wakiwemo wafanyabiashara wanaoweza kuwasilisha malalamiko yao kwa hasira.
Ameongeza kuwa lugha nzuri katika utoaji wa huduma hujenga uaminifu, huvutia wateja na kuwafanya wafanyabiashara kuendelea kutumia huduma za soko hilo.
“Ukiwa na lugha nzuri, mteja atarudi tena. Tunataka Soko la Kariakoo liwe soko la mfano. Katika Wiki ya Huduma kwa Wateja, tujifunze kutoa huduma kwa usahihi, heshima na staha,” amesema.
Aidha, amewataka watumishi kuhakikisha maombi na changamoto zinazowasilishwa zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati, huku wafanyabiashara wakisisitizwa kuuza bidhaa bora ili kuvutia wateja wa ndani na nje ya nchi.
Katika hatua nyingine, Charangwa amewataka wafanyabiashara kuimarisha usafi katika maeneo yao ya biashara na kusafisha mifereji inayowazunguka ili kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa zinazotarajiwa kunyesha.
Amesema usafi ni jukumu la kila siku na kuwataka wafanyabiashara kuhakikisha kila mmoja anakuwa na kifaa cha kutunzia taka katika eneo lake la biashara.
Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko ya Kariakoo, CPA Ashraph Abdulkarim, amesema kituo hicho kimeanzishwa ili kuwapa wafanyabiashara nafasi ya kuwasilisha changamoto zao na kutoa tathmini kuhusu ubora wa huduma zinazotolewa na watumishi wa shirika hilo.
Amesema wafanyabiashara wanaweza kutumia kituo hicho kuripoti changamoto mbalimbali, ikiwemo zinazohusu vizimba vya biashara na huduma nyingine zinazotolewa sokoni hapo.
“Soko la Kariakoo ni kitovu cha biashara. Mwenye changamoto tuko hapa tutawasikiliza. Iwapo kizimba chako kimechukuliwa, utatupigia,” amesema Abdulkarim.
Amewataka wafanyabiashara kushirikiana na shirika hilo katika kulinda miundombinu ya soko iliyojengwa kwa gharama ya zaidi ya Sh bilioni 28, akieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuhakikisha mazingira ya biashara yanaendelea kuwa bora.
Abdulkarim amesema uzinduzi wa kituo hicho ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan, aliyewahi kulitaka shirika hilo kujikita katika matumizi ya mifumo ya kidijitali katika utoaji wa huduma.
Amesisitiza kuwa watumishi wanapaswa kujiepusha na mabishano na wateja na badala yake kutumia weledi katika kushughulikia malalamiko na mahitaji yao.
“Hivi karibuni kumekuwa na tukio kati ya mtumishi na mteja wakijibizana. Tunafahamu kuwa mtumishi amepata elimu na amefundishwa namna ya kumhudumia mteja, hivyo anapaswa kutoa huduma kwa weledi bila bughudha,” amesema.
Amesema wafanyabiashara wanaweza kupiga simu bila malipo kupitia namba 0800114040 kwa saa 24 kwa siku, akieleza kuwa huduma hiyo itapatikana hata siku za Jumapili.
Aidha, Abdulkarim amesema utafiti uliofanywa na shirika hilo kwa kuwahoji wafanyabiashara umeonesha kuwa huduma zinazotolewa zinakubalika kwa zaidi ya asilimia 70, huku usafi ukiwa miongoni mwa huduma zilizotajwa kuridhisha wafanyabiashara.







