Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Handeni
KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Wazo Mwang’onda, amewaelekeza Wakurugenzi wa Halmashauri za Majiji, Miji na Wilaya nchini, kuwekeza zaidi katika usimamizi wa miradi na huduma za maendeleo, ili kufikia kusudio la kuinua hali ya maisha na ustawi wa watu.
Mwang’onda ametoa rai hiyo jana wakati akizungumza na wakazi wa Halmashauri ya Mji Handeni, wakati Mwenge wa Uhuru ulipotembelea, kukagua, kuweka jiwe la msingi, kufungua na kuzindua miradi mbalimbali kwenye halmashauri hiyo.
Miradi iliyohusika kwenye mbio za Mwenge wa Uhuru wenye ujumbe unaosema ”Tanzania ni yetu sote, tushikame kwa pamoja kuleta maendeleo” ni maji Kwamaizi, Brightness Shoppers na maabara kwenye Hospitali ya Halmashauri.
Mingine ni ujenzi wa madarasa mawili na ofisi katika Shule ya Sekondari Konje, ofisi ya mtaa wa Kwedisewa, mradi wa kuosha magari Zizini na barabara ya Chanika Kilole yenye urefu wa kilomita 1.7.
Akiwa katika Shule ya Sekondari Konje ambapo Mwenge uliweka jiwe la msingi ujenzi wa madarasa mawili na ofisi moja, Mwang’onda alisema Serikali ya Mhe. Rais Dkt. Samia inatoa fedha nyingi kufanikisha miradi ikiwemo ya elimu yenye lengo la kuwaandaa vijana kuwa wataalamu bora wa baadaye nchini.
Alisema fedha hizo zinatumika kwa ujenzi wa miundombinu, vifaa vikiwemo vya tiba (afya), kujifunza na kujifunzia kwenye taasisi za elimu, hivyo umuhimu wa usimamizi wa karibu na weledi kwa Wakurugenzi ni jambo lisiloepukika.
“Hizi ndizo salaam za Mwenge wa Uhuru kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini,” amesema Mwang’onda.
Pia, Mwang’onda ametoa rai kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa, kuhakikisha majukwaa ya vijana yaliyozinduliwa kwenye halmashauri wakati wa mbio za Mwenge, yanakuwa endelevu na kushushwa hadi ngazi ya kata.
Amesema hatua hiyo itawezesha kufikisha huduma, mipango na miradi ya kiuchumi kwa vijana wengi zaidi na hivyo kufikisha maendeleo kwa kada hiyo na jamii kwa ujumla.
Taarifa ya miradi kwa Mwenge wa Uhuru ilioenesha kuwa, ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika zahanati ya Magamba ulioanza Mei 4, 2021 kwa nguvu za wananchi umegharimu Shilingi milioni 15.8 hatua iliyofikiwa sasa.
Pia, taarifa hiyo ilieleza kuwa, jengo kama hilo kwenye zahanati ya kijiji cha Tuliani-Kwachaga,limegharimu Shilingi milioni 27.9 ambapo Shilingi 5,546,000.00 ni thamani ya nguvu za wananchi.


