Na Alex Kazenga

Dar es Salaam

Julai Mosi, 2022 Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA JKT) litatimiza miaka 41 ya kuasisiwa kwake huku likipania kutumia uzoefu wake kutanua shughuli zake hadi nje ya nchi.

Linakusudia kutumia uhusiano mzuri uliopo baina ya Tanzania na nchi majirani, hasa za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kutimiza azima hiyo, likilenga kuongeza wigo wa masoko ya shughuli na bidhaa zake.

Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa SUMA JKT, Kanali Petro Ngata, anasema maadhimisho yao ya kutimiza miaka 41 yatafanyika sambasamba na Maonyesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) katika viwanja vya

Mwalimu Julius Nyerere yatakayoanza rasmi Juni 28 hadi Julai Mosi, 2022.

“Kilele cha maadhimisho ni Julai Mosi, mwaka huu na mgeni rasmi atakuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Stergomena Tax.

“Nawakaribisha wadau mbalimbali kufika viwanja vya Sabasaba kuona shughuli mbalimbali zinazofanywa na SUMA JKT kwenye banda la JKT,” anasema Kanali Ngata huku akijivunia kuchangia pato la taifa na kutoa kodi stahiki serikalini kupitia kampuni tanzu walizoanzisha.

Ngata anasema SUMA JKT imefanikiwa kutekeleza miradi mbalimbali ukiwamo ujenzi wa ukuta kuzunguka mgodi wa madini ya tanzanite eneo la Mirerani mkoani Manyara na ujenzi wa mji wa serikali jijini Dodoma kuwa yenye manufaa

makubwa kwa taifa.

Mbali na hilo, anasema shirika linajivunia kusaidia utatuzi wa tatizo la ajira nchini, hasa kwa vijana kwa kupitia Kampuni ya ulinzi ya SUMA JKT Guard wameajiri vijana zaidi ya 16,000.

“Miaka 41 ya kuanzishwa kwa shirika tumefanikiwa kusaidia vijana wanaojiunga JKT kupata mafunzo ya stadi za kazi.

“Kupitia shughuli za uzalishaji za shirika vijana wamepata stadi za kuendesha shughuli za kilimo, ujenzi, utengenezaji wa samani na bidhaa za ngozi,” anasema Kanali Ngata.

Mafanikio yaliyofikiwa

Idara ya Habari na Uhusiano kwa niaba ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa SUMA JKT, Meja Jenerali Rajabu Mabele, wanaelezea mafanikio ya shirika hilo tangu kuanzishwa kwake mwaka 1981 kuwa ni mengi na wanasifia kuwa na uwezo

mkubwa wa kubuni miradi mipya inayotoa fursa za ajira ndani ya jamii.

Huku faida inayopatikana kutokana na kampuni tanzu na miradi ya shirika hilo imesaidia kwa kiwango kikubwa katika shughuli za malezi ya vijana kwa kuchangia gharama za kuendesha mafunzo ya vijana wanaojiunga JKT.

Pia inajivunia kutoa mafunzo ya stadi za kazi kwa vijana wanaojiunga na mafunzo ya JKT mara baada ya kupata mafunzo ya awali ya kijeshi.

Mafunzo hayo ni pamoja na ushonaji, ufundi seremala, ushonaji viatu, ufugaji samaki kwa njia ya matanki na vizimba pamoja na ujenzi.

Wakati SUMA JKT ikisherehekea miaka 41 ya kuasisiwa kwake, inajivunia kutekeleza mradi wa kujenga nyumba 41 katika Ikulu ya Chamwino na ujenzi wa majengo ya wizara sita katika mji wa serikali Dodoma iliyotekelezwa mwaka 2020.

Pia inajivunia kujenga jengo la Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) katika mji huo, ujenzi wa Ofisi za Rais – Ikulu, Chamwino na uzio wake wenye urefu wa kilomita 27.

Miradi mingine ni ujenzi wa wodi za watu mashuhuri katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), wodi za wajawazito katika Hospitali ya Rufaa Mbeya na ujenzi wa Hospitali ya Uhuru iliyopo Chamwino, Dodoma.

Mbali na miradi hiyo, imehusika katika ujenzi wa madarasa na mabweni katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, Chuo cha Ualimu cha Kabanga kilichopo Kigoma na maabara mtambuka katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).

Pia imefanikiwa kuboresha viwanda vilivyopo na kuanzisha vipya na hatua hiyo ikitajwa kuwa ya kuunga mkono juhudi za serikali za kufikia uchumi wa kati wa viwanda ifikapo mwaka 2025.

Viwanda vinavyomilikiwa na SUMA JKT kwa sasa ni SUMA JKT Garments Co. Ltd, SUMA JKT Chang’ombe Furniture Co. Ltd, SUMA JKT Leather Products, SUMA JKT Bottling Co. Ltd na SUMA JKT Mlale Mills Co. Ltd.

Mipango ya baadaye ya SUMA JKT

Mipango yake ni kuboresha huduma zilizopo na kuanzisha huduma nyinge mpya. Maeneo inayokusudia ni sekta ya ujenzi, uhandisi na ushauri majenzi na kukuza uzoefu kupitia miradi ya kimkakati inayotekelezwa nchini.

Kupitia miradi hiyo, inakusudia kuwaongezea uzoefu watendaji wake kwa kuongeza ushirikiano na kampuni za kimataifa kutoka nje ya nchi yenye uzoefu mkubwa na kumiliki teknolojia za kisasa.

Pia inakusudia kuongeza wigo katika huduma za ushauri hasa katika huduma za ardhi kwa kuzingatia mipango miji, upimaji na uthaminishaji wa ardhi na huduma za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kwa ujumla.

Vilevile imepanga kutanua wigo wa masoko kwa kutekeleza shughuli za ujenzi, uhandisi na ushauri nje ya nchi, hasa katika nchi za EAC.

Malengo mengine yanaelekezwa katika kuongeza uzalishaji wa mbegu bora za kilimo kwa kutumia mashamba yake ya kuzalisha mbegu kwa kutumia Kampuni ya SUMA JKT Seeds Company Ltd.

Pia katika kutimiza hilo itashirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI), Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu (TOSCI) na SUA).

Katika hatua nyingine, inapanga kutumia teknolojia ya kisasa ya mitambo katika miradi yake ya mifugo na uvuvi.

Kwa kutumia teknolojia hiyo, itaboresha uandaaji wa chakula cha mifugo, udhibiti wa magonjwa na utunzaji wa mazao ya nyama, ikiwa ni pamoja na kufanya uvuvi bahari kuu bila kuathiri mazingira.

Historia ya kuanzishwa SUMA JKT

Wazo la kuanzishwa SUMA JKT lilianza miaka ya 1970 baada ya Mwalimu Julius Nyerere kutembelea makambi mbalimbali ya JKT kujionea shughuli za mafunzo, malezi ya vijana na uzalishaji mali na kubaini kasoro kadhaa.

Mwalimu Nyerere alibaini katika baadhi ya makambi shughuli za mafunzo, malezi ya vijana na uzalishaji mali zimeathiriwa na ucheleweshwaji wa fedha za uendeshaji wa JKT, hali iliyosababisha malengo kutofikiwa jinsi ilivyotakiwa.

Katika kutatua tatizo hilo ndipo Mwalimu Nyerere akatoa wazo la kuanzishwa SUMA JKT. Baada ya wazo hilo kupitia katika hatua mbalimbali za serikali na kutathminiwa, mwaka 1981 serikali kupitia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la

Kujenga Taifa ilizindua rasmi SUMA JKT.

By Jamhuri