Mabomu Mbagala siri zavuja

Tathmini ya tatu
Baada ya kutokea mkanganyiko huo huku wananchi wengi wakionyesha kutoridhishwa na majibu yanayotolewa na Serikali, kwa mara ya tatu Serikali iliamua kurudia tathmini iliyoanza Januari 19, 2010. Watu wapatao 1,438 walikuwa wakilalamika kupunjwa malipo yao, huku waathirika 601 wakidai kurukwa kwa makusudi katika uthamini.

“Serikali ilitoa jumla ya shilingi 516,393,360 ili kuwezesha utekelezaji wa kazi ya tathmini ya awamu ya kwanza na ya pili pamoja na jumla ya shilingi 259,791,750 ili kuwezesha utekelezaji wa kazi ya tathmini ya awamu ya tatu,” inasema sehemu ya taarifa ya Serikali kwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali iliyowasilishwa wiki iliyopia.

Baada ya kutumia mamilioni hayo kufanya uhakiki kuanzia Julai 28, 2010, yalifanyika malipo ya awamu ya tatu kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu ambapo kiasi cha Sh 1,144,508,000 zimetumika kulipa fidia waathirika 993. Kati ya waliokuwa wameachwa nje ya malipo, waathirika 486 walilipwa wastani wa Sh 270,532,000 kwa ujumla wao.

Kwa watu wote waliofariki ambao jumla kuu ni 29, kila familia ililipwa wastani wa Sh milioni 10 zilizotumika kwa ajili ya mazishi na ubani kwa familia. Hii inajumuisha raia 20, askari sita na watoto watatu waliolipukiwa na masalia ya mabomu.