Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Dkt.Angeline Mabula amesema kuwa uwekezaji katika sekta ya nyumba unahitaji kiwango kikubwa Cha fedha hivyo benki na taasisi za fedha zina mchango mkubwa katika kukuza sekta ya nyumba nchini.

Hayo ameyasema wakati wa hafla ya utiliaji saini wa mkataba makubaliano kati ya Benki ya Absa Tanzania na NHC wenye lengo la kuwawezesha Watanzania kupata mikopo ya nyumba za Shirika hilo iliyofanyika katika eneo ulipo mradi mkubwa wa nyumba za NHC zilizopo Morocco Square jijini Dar es Salaam.

“Kwa kiasi kikubwa uwekezaji sekta ya nyumba umechangia ukuaji wa ajira,kipato, mitaji na kuimarisha afya na elimu hivyo Serikali zote duniani zinaheshimu mchango wa sekta za nyumba katika kukuza uchumi.

“Pia uwekezaji sekta ya nyumba ni kichocheo kikubwa cha kudumisha amani, hivyo ni dhahiri kwamba hakuna nchi inayoendelea duniani bila kutoa kipaumbele kwa sekta ya nyumba”amesema Dkt.Mabula.

Mabula amesema kuwa makubaliano kati ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na Benki ya ABSA Tanzania una lengo la kuwawezesha Watanzania kupata mikopo ya nyumba za shirika hilo pia itakuwa chachu kubwa ya Watanzania kumiliki nyumba kwa njia za mikopo..

“Ninapongeza hatua hii kwani itakuwa ni manufaa makubwa kwa wateja wa Benki ya Absa, Shirika la Nyumba la Taifa pamoja na wanunuzi wa nyumba hizo,” amesema Mabula.

Dkt.Mabula ameongeza kuwa nia ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ni kuona Serikali na sekta binafsi zinashirikiana katika kuondoa changamoto ya uhaba wa nyumba kwa Watanzania wote kwa kuhakikisha wanakuwa na nyumba za kisasa na wanakuwa na nyumba bora hivyo mpango huo wa ABSA na NHC utatoa fursa za wananchi kupata mikopo ya nyumba.

Hata hivyo ametoa wito kwa benki na taasisi za kifedha zinazotoa mikopo ya nyumba hapa nchini kutafuta mbinu za kuwezesha mikopo hiyo iwe na riba nafuu ili kuwawezesha hata wananchi wenye kipato cha chini waweze kumudu gharama hizo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemia Mchechu, amesema shirika hilo litashirikiana vyema na benki ya Absa katika utoaji wa nyumba za kisasa kwa wateja watakaokopa nyumba hizo kupitia benki hiyo.

Amesema kuwa shirika hilo litawajengea nyumba wateja wake ambao walinununua viwanja vyao kwenye shirika hasa miradi ya Safari City iliyopo Arusha mara baada ya wateja hao kupata mikopo ya ujenzi wa nyumba kupitia benki ya Absa.

Mchechu ameongeza kuwa miradi wa Samia Housing Scheme itatekelezwa kwa nchi nzima na wameanza na eneo la Kawe jijini Dar es Salaam ambapo asilimia 70 ya mradi huo imepata wateja.

Ameongeza kuwa shirika hilo lina mpango wa kuifanya Kawe kuwa mji wa kisasa ambao utaendesha shughuli zake kwa saa 24 na hata eneo kubwa la michezo hapa nchini (sports Arena)itaanza kujengwa eneo la Kawe.

Mchechu ameongeza kuwa kupitia ushirikiano wa kibiashara kati ya Absa na NHC sasa wateja wa NHC hawapaswi kuwa na hofu kwani watapata mikopo yenye riba nafuu ambayo itawawezesha kununua nyumba za shirika hilo huku akitoa wito kwa Watanzania waishio nje ya nchi (diaspora) kutokuwa na shaka ya kupata nyumba za shirika hilo kupitia benki hiyo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania amesema kuwa baada ya benki hiyo kufanya tafiti wamegundua kuwa Watanzania wamekuwa wakihangaika kupata mikopo kwa ajili ya kununua au kujenga nyumba za kisasa hivyo kupitia mkataba huo Watanzania wataweza kumiliki nyumba za kisasa kwa gharama nafuu.

By Jamhuri