Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA),inapenda kutoa ufafanuzi juu ya taarifa za uwepo wa kimbunga ‘Freddy’ zinazosambaa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii na kuzua taharuki kwa jamii.

Kupitia sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na. 2 ya mwaka 2019, Mamlaka imepewa jukumu kisheria kufuatilia na kutoa tahadhali za hali mbaya ya hewa kwa jamii. Taarifa hizi za hali mbaya ya hewa hutolewa kwa jamii pale tu zinapokuwa zimekidhi viwango na miongozo ya utendajikazi.

Kwa takribani wiki sasa Mamlaka imekuwa ikifuatilia mwenendo wa kimbunga “Freddy” kilichopo kusini magharibi mwa bahari ya Hindi karibu na pwani ya Madagascar na kujiridhisha kutokuwa na madhara ya moja kwa moja kwa sasa kwa maeneo yaliyoko nchini kwetu.

Mamlaka ya hali ya Hewa Tanzania,inaendelea kufuatilia kwa kina mwenendo wa kimbunga hiki na itatoa taarifa punde tu kutakapokuwa na haja ya kufanya hivyo.

Aidha,Mamlaka inapenda kuikumbusha jamii na umma kwa ujumla kuwa kwa mujibu wa sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na. 2 ya 2019, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ndiyo pekee yenye mamlaka ya kutoa taarifa za tahadhari za matukio ya hali mbaya ya hewa na ni kosa kisheria mtu mwingine kufanya hivyo.

Kwa taarifa hii wananchi wanashauriwa kuendelea kuzingatia taarifa na tahadhari za hali mbaya ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania sambamba na kutafuta, kupata na kufuata ushauri wa wataalam katika sekta husika ili kupunguza athari zinazotokana na hali mbaya ya hewa.

By Jamhuri