Mabula awataka Ma-DC kuanzisha rejista ya migogoro ya ardhi

Waziri wa ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angelina Mabula amewataka Wakuu wa Wilaya nchini kuhakikisha kila Halmashauri inakuwa na rejista ya migogoro ya ardhi ili kujua chanzo chake pamoja na mikakati ya utatuzi wa migogoro hiyo kila inapojitokeza.

‘’Natambua kuwa kila Mkuu wa Wilaya anapoteuliwa migogoro ambayo ishapatiwa ufumbuzi uwa inaanza upya ndio maana nawataka kusimamia uanzishwaji wa rejista ya migogoro ya ardhi itakayosimamiwa na wakurugenzi ili kudhibiti na kumaliza migogoro ya ardhi.’’amesema Dkt. Mabula.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula

Waziri Mabula amesema hayo jana wakati wa uwasiliajishaji wa mada yake kwa wakuu wa Wilaya wanaoshiriki mafunzo yanayoendelea Jijini Dodoma chini ya Ofisi ya Rais TAMISEMI.

Katika mada yake hiyo Dkt. Mabura alisema kumekuwepo na changamoto kwenye halmashauri ya kutodhibitiwa kwa migogoro ya ardhi na kutosimamia mipango ya matumizi ardhi iliyoandaliwa mijini na vijijini.

Changamoto nyingine aliyoisema Waziri Mabula ni Halmashauri kutoshiriki kikamilifu kwenye mikakati ya makusanyo yanayotokana na sekta ya ardhi pamoja na bajeti ndogo ya kutekeleza majukumu ya sekta na kutokutengwa kwa ardhi ya uwekezaji.

Aidha Waziri huyo aliwataka viongozi hao wa Wilaya kusaidia katika kuongeza hamasa kwenye suala la ukusanyaji wa mapato ya serikali yanayotokana na sekta ya ardhi ikiwemo kusimamia mikakati ya ukusanyaji maduhuli na kuwakumbusha wananchi kutumia fursa iliyotolewa na Rais ya msamaha wa malimbikizo ya kodi ya pango la ardhi inayoishia tarehe 30 Aprili, 2023.

Baadhi ya Wakuu Wilaya wakifuatilia mada iliyotolewa kwao na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula jana Jijini Dodoma.

Waziri Mabula amewataka viongozi hao wa Wilaya kusimamia Halmashauri ili zitenge fedha kwenye Bajeti ili kuhakikisha ardhi inapangwa, kupimwa na kumilikishwa huku akiwahimiza kutambua kuwa mamlaka za upangaji ardhi ziko chini ya Halmashauri.

‘’Halmashauri zitambue kuwa jukumu hilo bado ni lao na wanahitaji kuendelea kushiriki kikamilifu kwenye kutenga fedha ili kutekeleza majukumu yao na kuwawezesha watumishi waliopo katika Halmashauri kufanya kazi kwa mujibu wa taaluma zao’’ ameongea Waziri Mabula.

Waziri Mabula pia alidokeza kuwa kuna baadhi ya Halmasahauri Nchini ambazo zimetumia mikopo ya 50M. iliyotolewa na Rais kwa baadhi ya Halmashauri ili zitumike Kupima, Kupanga na Kumilikisha ardhi lakini baadhi ya Halmashauri zilielekeza fedha hizo katika matumizi mengine bila kuzingatia kusudio la mikopo hiyo.

Kwa mukutadha huo Waziri Mabula alielekeza Wakuu wa Wilaya kusimamia eneo hili ili wakurugenzi wa Halmashauri watumie mikopo hii kwa ajili ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi na hatimaye kurejesha fedha hizo ili Halmashauri nyingine ziweze kukopeshwa.