MAHAKAMA YAANZA UJENZI WA MAHAKAMA TATU MKOANI GEITA

IMG_7723
Jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Geita na Mahakama ya Wilaya Geita likiwa katika hatua za awali za ujenzi 
IMG_7739
Jengo la Mahakama ya Wilaya ya Bukombe likiwa katika hatua za awali za ujenzi wake katika mji mdogo wa Ushirombo wilayani Bukombe
IMG_7742
Jengo la Mahakama ya wilaya ya Chato likiwa katika hatua ya Msingi. Majengo haya yote yanajengwa kwa Teknolojia ya Gharama nafuu na ya muda mfupi iitwayo Moladi na yanajengwa na Kampuni ya Moladi Tanzania. Ujenzi wake unatarajiwa kutumia muda wa miezi sita.
Katika kutekeleza dhamira yake ya kuboresha huduma za Mahakama na kusogeza huduma hizo karibu zaidi na wananchi, Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Dunia imeanza rasmi ujenzi wa majengo matatu ya Mahakama katika mkoa wa Geita pamoja na wilaya zake za Bukombe na Chato.
Ujenzi wa Mahakama hizi ni utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano (2015/16 hadi 2019/2020) wa Mahakama ya Tanzania pamoja na Mradi wa Maboresho ya Huduma za Mahakama ambao ulianza kutekelezwa rasmi mwaka 2015. Miradi hii kwa pamoja inalenga kuboresha huduma na kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.
Mahakama imeanza ujenzi wa jengo la Mahakama ya Mkoa wa Geita ambalo litajumuisha pia na Mahakama ya wilaya ya Geita. Majengo mengine yanayojengwa ni ya Mahakama za wilaya za Bukombe na Chato.
Majengo haya yanatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi sita kutoka sasa na yanajengwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa na gharama nafuu na ya muda mfupi iitwayo Moladi ambapo kampuni ya Moladi Tanzania ndiyo imepewa dhamana ya kujenga majengo hayo. Jumla ya majengo ya Mahakama za Mkoa, wilaya na Mwanzo sita tayari yameshajengwa kwa kutumia teknolojia ya Moladi katika jiji la Dar es salaam na Mkoa wa Pwani.
Majengo haya ni yale ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Pwani na Mahakama ya Wilaya ya Kibaha, Mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo, Kigamboni, Mkuranga pamoja na jengo la Mahakama ya wilaya ya Kigamboni na Mahakama ya Mwanzo Kigamboni na Mahakama ya Mwanzo Kawe jijini Dar es salaam.
Mhandisi wa Kampuni ya Moladi Tanzania anayesimamia ujenzi wa Mahakama za Geita, Bukombe na Chato, Camilius Mihambo akielezea ujenzi wa Mahakama hizo alisema ujenzi huo unaendelea vizuri na kazi hiyo inatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi sita kilichopangwa . Mhandisi Mihambo amesema hatua ya ujenzi iliyofikiwa sasa ni hatua ya awali ya kujenga msingi katika majengo yote matatu.
“Kazi kubwa na inayochukua muda mrefu kwa sasa ni ya kujenga msingi, hatua inayofuata ya kuweka ukuta ni ya muda mfupi kwa kuwa tunatumia teknolojia ya Moladi ambayo kuta zinaweza kusimama ndani ya siku tatu na kuendelea, alisema Mhandisi huyo.
Akizungumzia hatua ya Mahakama ya Tanzania kuanza ujenzi katika Mkoa wa Geita, Mtendaji wa Mahakama ya Mkoa wa Geita, Lothan Simkoko anaelezea kufurahishwa kwake kwa uamuzi wa Mahakama kujenga Majengo ya Mahakama za wilaya na Mkoa katika mkoa wa Geita. Anasema ujenzi huo utasaidia upatikanaji wa haki kwa wakati kwa wananchi wanaofika Mahakamani kutafuta haki zao pia kumaliza changamoto ya ufinyu wa ofisi. Alisema, jengo la Mahakama ya Mkoa litakapomalizika litatoa nafasi zaidi na kuboresha huduma. Mahakama ya Mkoa wa Geita ina upungufu wa chumba cha Mahabusu, chumba cha kuhifadhi ushahidi pamoja na ofisi kwa ajili ya watumishi wake.
Mtendaji huyo alisema Mahakama Mkoani Geita haina jengo la Mahakama ya wilaya na badala yake jengo linalotumika sasa kwa Mahakama ya wilaya na Mwanzo ni la kuazima na pia haliko katika hali nzuri. Alisema kukamilika kwa jingo jipya la Mahakama mkoani humo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma za Mahakama.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi waliohojiwa juu ya ujenzi wa Mahakama hizo walionyesha kufurahishwa na hatua hiyo ya Mahakama kujenga majengo yake mapya. Bwana Mika Jonathan Shija ambaye ni Mkazi wa Geita anaelezea kufurahishwa kwake na ujenzi wa Mahakama ya Mkoa na ya Wilaya ya Geita na kusema kuwa ujenzi huo utakapokamilika utawarahisishia wananchi kupata huduma. “kama tulivyoambiwa kuwa Mahakama ya Mkoa na wilaya zitakuwa kwenye jengo moja hivyo kwetu sisi ni rahisi kwa kuwa itakuwa ni rahisi kutoka  sehemu moja kwenda nyingine”, alisema.
Naye Pili Malongo Mkazi wa Bukombe yeye alisema amefurahishwa na ujenzi wa Mahakama wilayani humo kwa kuwa anaamini jengo jipya la Mahakama litakuwa na sehemu iliyotengwa kwa ajili ya wananchi kupumzika wakati wakisubiri kupatiwa huduma mahakamani hapo.
Pamoja na ujenzi wa Mahakama hizo tatu katika Mkoa wa Geita, Mahakama ya Tanzania tayari imeanza kutekeleza program ya ujenzi wa majengo 18 ya Mahakama katika mwaka huu wa fedha wa 2017/2018 anabainisha Mkuu wa Kitengo cha Majengo (Estate Management) wa Mahakama ya Tanzania Mhandisi Khamadu Kitunzi.
Kwa mujibu wa Mhandisi Kitunzi, kati ya majengo 18 yaliyoanza kujengwa nchini,  majengo mawili ni ya Mahakama Kuu yanayojengwa kwenye Mikoa ya Mara na Kigoma, matano ni ya Mahakama za Hakimu Mkazi yanayojengwa katika mikoa ya Geita, Njombe, Lindi, Simiyu, na Katavi. Aidha jumla ya majengo 11 ya Mahakama za Wilaya yanajengwa katika wilaya za Kasulu, Rungwe, Ruangwa, Kilwa Masoko, Kilindi, Sikonge, Kondoa, Bunda na Longido.
Aidha, Mahakama pia imefanikiwa kujenga Mahakama za Mwanzo na pia kumalizia baadhi ya Mahakama zilizoanza kujengwa kwa nguvu ya wananchi katika maeneo mbalimbali nchini kama vile Itinje-Meatu, Robanda-Serengeti, Wasso-Loliondo, na Karatu Arusha. Maeneo mengine ni Beleko-Kondoa, Mahakama ya Old Korogwe-Korogwe, Mvomero Morogoro, Mahakama ya Mwanzo Totoe iliyopo Mkoani Songwe na Mahakama ya Mwanzo Iguguno mkoani Singida.
Akifafanua zaidi kuhusu ujenzi wa majengo ya Mahakama, Mhandisi Kitunzi anaeleza kuwa hivi sasa zipo Mahakama Kuu 14 na baada ya kukamilika kwa ujenzi wa Mahakama kuu katika mikoa ya Mara na Kigoma kutakuwa na jumla ya Mahakama kuu 16 nchini na kubaki na uhitaji wa Mahakama Kuu 10 katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara. Mahakama ya Tanzania inalenga kujenga majengo ya Mahakama kuu ambayo yatatumika kama Kituo Jumuishi cha kutoa huduma za kimahakama yaani Intergrated Justice Centre. Mahakama tayari ilifanya ukarabati mkubwa wa jengo la Mahakama Kuu kanda ya Mbeya ambapo hivi sasa Mahakama hiyo inafanya kazi kama kituo Jumuishi cha huduma za Kimahakama.
Mhandishi Kitunzi anasema Mahakama inao mpango wa kujenga Majengo ya Mahakama Kuu ambayo yatatoa huduma kama kituo Jumuishi cha kutoa Huduma za Kimahakama kwa kushirikiana na Benki ya Dunia katika mikoa ya Dar es salaam, Morogoro, Dodoma, Singida, Mwanza na Arusha.