Majambazi wajitangazia Serikali

*Wajiundia Jeshi la Ukombozi la Wana Sonjo

*Wabuni bendera, mahakama na polisi yao

*Vijiji vyawatii, waendesha ujangili, ujambazi


Watu wanaokadiriwa kuwa zaidi ya 500 wanaodhaniwa kuwa ni majambazi na majangili, wamejiundia serikali ndani ya Msitu wa Igombe mkoani Tabora, JAMHURI inathibitisha.

Wamejiundia uongozi madhubuti pamoja na jeshi walilolipa jina la Jeshi la Ukombozi la Wana Sonjo.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa huenda idadi ya watu hao ikawa kubwa kuliko inavyodhaniwa, kwani wanadaiwa kusambaa ndani ya misitu minene katika mikoa ya Tabora na Shinyanga. Pia wapo katika maeneo kadhaa ya Mkoa wa Kigoma.

Imebainika kuwa watu hao wapo katika Msitu wa Igombe uliopo wilayani Uyui na kusambaa katika mapori mengine ya Malagarasi na Myowosi; na walianza kujiimarisha tangu mwaka 2010.

Duru za uchunguzi zimebaini kuwa wanaounda ‘serikali’ hiyo wanatoka katika makabila kadhaa ya mikoa ya Tabora, Shinyanga, Arusha, Kigoma na katika mataifa jirani, hasa Burundi.

“Serikali” hiyo batili ina jeshi lake la ulinzi, jeshi la polisi, mahakama na vyombo vingine vya utawala.

Shughuli kuu zinazofanywa ni ujambazi, ujangili, kilimo cha bangi, biashara ya mbao, uuzaji bunduki pamoja na risasi; na uhalifu wa aina nyingine.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Fatuma Mwasa, amezungumza na JAMHURI na kusema, “Ni kweli tuna tatizo hilo. Lipo na ni kubwa. Serikali imeshalitambua, na hatua zinachukuliwa.”

Mwasa, licha ya kukiri, hakutaka kuingia kwenye undani wa suala hilo katika kile kinachoonekana kuwa ni kutotaka kutibua hatua za kiusalama zilizopangwa kuchukuliwa na vyombo vya dola katika kukabiliana na genge hilo.

Hata hivyo, maneno ya Mwasa katika kuthibitisha ukubwa wa jambo hili ni haya, “Kweli tatizo lipo…ni kubwa kuliko unavyofikiri.”

Watu wawili waliokamatwa na baadaye kutoroka kutoka mikononi mwa kundi hilo wamesema genge hilo ni masalia ya wale walioshughulikiwa na Serikali mwaka 2010. Majina ya watu hao tunayahifadhi kutokana na sababu za usalama wao.

“Kuna jeshi lenye askari wa jadi wenye bunduki za SMG (Sub Machine Gun), na magobore. Wanaendesha uasi. Wamepandisha bendera ya bluu, imeandikwa Jeshi la Ukombozi la Wana Sonjo. Wahalifu wengi wageni wanatoka Burundi. Wanashirikiana na Wasonjo, Wasukuma na Waha.

“Shughuli zao ni kilimo cha bangi, kupasua misitu, uwindaji haramu na n.k. Wana watemi wao. Kila mtemi analindwa na askari wasiopungua 20,” anasema mmoja wa watoa habari wetu.

Uimara wa magenge hayo ya wahalifu yaliyojiimarisha yamewafanya hata wananchi na viongozi wa vijiji jirani na mapori wanamoishi, wawe watiifu kwao.

“Ukiwa na tatizo unaenda msituni kuomba msaada wa askari kukukamatia mhalifu au mbaya wako. Wanatumwa askari wanakuja kukuteka na kukupeleka huko msituni.

“Ukienda kushitaki unalipa hela. Kama unahitaji huduma…kama unamdai mtu, kama ulimkopesha ng’ombe na yeye hataki kukulipa unakwenda msituni, unaonana na makamanda, unaonana nao, wanaleta watu wao wanakuteka. Wanakupeleka hadi msituni, unaadhibiwa. Huachiwi hadi ndugu wapeleke ng’ombe au hela ndiyo uachiwe,” anasema.

Ukatili huo umegeuzwa kuwa mradi wa baadhi ya viongozi wa vijiji vinavyopakana na mapori hayo.

“Tulipokuwa kule tuliwaona watu wa kutoka Arusha (Wasonjo). Hawa wanashughulika zaidi na kilimo cha bangi. Warundi wanapeleka silaha na risasi. Wanazitoa kwao ambako kuna mapigano. Wengine ni wale waliotoroka kwenye kambi za wakimbizi. Wanashirikiana na raia.

“Risasi zinauzwa kwenye ndoo kama karanga. Hali ni mbaya. Ukiwa kule huwezi kujua kama uko Tanzania, unajiona uko katika utawala wa serikali nyingine kabisa,” amesema mtoa taarifa wetu.

Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso, alipoulizwa, aliomba aulizwe Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora.

“Naomba umwulize Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, tunapokuwa na RPC mahali ndiye anayekuwa mwakilishi wetu. Muulize atakupa taarifa,” alisema Senso.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi (RPC) wa Tabora, Suzan Kaganda, alipoulizwa na JAMHURI, hakutaka kukiri wala kukanusha juu ya uwepo wa genge hilo.

“Naomba uzungumze na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa (Mwasa). Kwa jambo kama hili yeye ndiye msemaji. Lakini nadhani ungeliacha kwanza ili RC alishughulikie. Zaidi ya hayo siwezi kusema lolote, naomba uwasiliane tu na RC,” alisema.

RPC Kaganda amewatoa hofu wananchi akisema Jeshi la Polisi lipo imara na hivyo waendelee na shughuli zao kama kawaida.

“Tuko imara, muhimu tunaomba ushirikiano wao katika ile dhana ya ulinzi shirikishi,” alisema.

Operesheni ya kuwaondoa itafanikiwa?

Duru za uchunguzi kutoka ndani ya Serikali zinasema viongozi na wataalamu mbalimbali kutoka vyombo vya ulinzi na usalama wamekuwa wakikuna vichwa kukabiliana na genge hilo.

Tayari makachero kadhaa wameshapelekwa kupeleleza nguvu za kijeshi na silaha walizonazo, na sasa kinachosubiriwa ni idhini kutoka kwa viongozi wahusika ili kuanza kwa operesheni.

Awali, operesheni hiyo ilipangwa iongozwe na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), lakini kuna taarifa kuwa kabla ya kuwatumia makamanda na wapiganaji kutoka jeshi hilo, ni vema wakaanza askari polisi wenye mafunzo madhubuti ya kukabiliana na matukio ya aina hiyo. Tayari fungu la fedha kwa ajili ya kazi hiyo limesharidhiwa, na kinachosubiriwa ni kuanza kazi wakati wowote.

Kigugumizi kinachowapata viongozi wa ulinzi na usalama ni maneno yanayoweza kutolewa na wanasiasa, hasa wabunge pamoja na wale wanaojiita kuwa ni watetezi wa haki za binadamu.

“Wabunge ndiyo wanaovuruga mambo, hii operesheni inafanywa kwa nia njema ya kuilinda nchi yetu, lakini hofu inayotupata ni kwamba tukishaanza tu, basi kelele nyingi zitapigwa. Wabunge wanapaswa kuelewa kile kitakachofanywa pale. Waache Serikali ifanye kazi yake. Tunataka Bunge lisilete balaa ya kuhoji au kulaani uamuzi huu ambao kimsingi ni uamuzi wa kuilinda nchi yetu na watu wake.

“Hakuna nchi ambayo watu wanaweza ku-compromise usalama wa nchi. Hakuna,” amesema mmoja wa viongozi wanaofuatilia suala hilo.

Msukosuko uliowapata viongozi wa Serikali na hata kufikia hatua ya mawaziri wanne kuondoka madarakani ulisababishwa na wabunge. Hali hiyo ndiyo inayowatia hofu viongozi wa Serikali; na vyombo vya ulinzi na usalama kuwa huenda safari hii wabunge wakaibuka tena na kushinikiza kuwajibika kwao.

Miaka kadhaa iliyopita, genge jingine kama hili lilijitangazia serikali yake katika misitu mkoani Tabora. Serikali ilianzisha operesheni na kulidhibiti.

Tukio jingine kama hilo liliwahi kutokea katika Tarafa ya Ingwe, Tarime mkoani Mara, mwanzoni mwa miaka ya 1980. ‘Waasi’ hao walipandisha bendera yenye picha ya chui, lakini hawakudumu muda mrefu kwani walikumbana na nguvu za dola.