Na Abel Paul wa Jeshi la Polisi

Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limemkamata Doreen Lema (30), mkazi wa Baraa katika Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa kosa la kumchoma pasi ya umeme mtoto wake wa kumzaa mwenye umri wa miaka saba katika maeneo mbalimbali ya mwili wake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishina msaidizi wa Polisi ACP Justine Masejo,ameyasema hayo leo Januari 31,2023 wakati akitoa taarifa wa vyombo vya habari,kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa na alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu mkazi Wilaya ya Arusha ambapo alikutwa na hatia na kuhukumiwa kifungo cha miaka mitano 5 kwenda jela kwa kosa la kumchoma mtoto na pasi.

Kamanda Masejo aliendelea kusema kuwa katika kuhakikisha jeshi hilo linaendelea kufuatilia vitendo vya ukatili wa watoto unaofanywa na baadhi ya watu katika mkoa huo litahakikisha linakomesha vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia na watoto.

Pia jeshi hilo limeendelea kushirikisha jamii na kutoa elimu ambapo limebainisha kuwa mkakati waliojiwekea umesaidia jeshi hilo na ofisi ya Taifa ya Mashtaka mkoani humo kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wanne na mahakama kuwakuta na hatia kwa makosa ya ubakaji.

ACP Masejo ametoa wito kwa wananchi kutojihusisha na vitendo vya ukatili wa aina yoyote ile kwani Jeshi la Polisi Mkoani hapa halito muonea muhali mtu yoyote atakaye bainika kwa makosa ya unyanyasaji vilevile Jeshi la Polisi linawaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa za vitendo hivyo.

Katika tukio lingine,Kamanda amesema wakazi wa wanne wa mkoani hapo wamehukiwa kwenda jela miaka 120 kwa kosa la ubakaji.

Masejo amewataja waliohukumiwa kuwa ni James Elorehema, John Sanare, Theophil Salaho, Japhet Mungure ambapo mahakama hiyo iliwakuta na hatia na kuwahukumu kifungo cha miaka 30 kwenda jela kila mmoja kwa kosa la ubakaji.

Pia katika tukio jingine kamanda Masejo amesema kuwa jeshi hilo limefanikiwa kukamata pikipiki iliyokuwa imeibiwa huko katika Kijiji cha Qangadend Wilaya ya Karatu ambapo mtuhumiwa Charles Jonas (27),mkazi wa Igunga mkoani Tabora alikamatwa akiwa na pikipiki yenye namba za usajili SM 12337 aina ya Boxer Mali ya Serikali ya Jamhuri ya Tanzania.

Aidha uchunguzi wa tukio hilo ulifanyika na mtuhumiwa alifikishwa katika mahakama ya Wilaya ya Karatu na kusomewa mashtaka yanayomkabili ambapo mahakama ilimkuta na hatia na kumhukumu kifungo cha miaka mitatu jela.

By Jamhuri