Mambosasa afunga mafunzo ya medani awaomba wananchi kutokuokota vitu vyovyote eneo la medani

Na Abel Paul, Jeshi la Polisi- Mkomazi,Tanga.

Jeshi la Polisi limewaomba wananchi wa maeneo ya karibu na kambi ya Jeshi la Polisi inayoendesha mafunzo ya mbinu za medani za kivita katika eneo la Mkundimbaru Mkomazi wilayani Korogwe Mkoa wa Tanga kutokuokota vitu vyovyote vyenye mfanano na Chuma na vile ambavyo wanashaka navyo na badala yake watoe taarifa kwa Jeshi hilo.

Hayo yamesemwa octoba 20, 2023 na Mkuu wa Chuo Cha Taaluma ya Polisi Dar es salaam (DPA) Kamishna msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Dkt Lazaro Mambosasa wakati akifungua mafunzo ya mbinu za medani za kivita kwa kundi la Maafisa na wakaguzi wasaidizi wanafunzi eneo la Mkomazi Mkoa wa Tanga.

Dkt. Mambosasa ameongeza kuwa endapo wananchi wataona kitu chochote chenye mfanano wa chuma au kipisi cha bomba wasiokote kama chuma chakafu huku akiwaomba wananchi hao kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ili wataalam wa milipuko wafike ili wavitambue kama ni vilipuzi vyenye kuleta madhara kwa binadamu.

Aidha amewataka maafisa na wakaguzi wasaidizi wanafunzi kuyapokea kikamilifu mafunzo hayo ambayo yatawaongezea mbinu za kimedani katika utendaji wa kazi za Jeshi hilo hasa kipindi hiki cha mabadiliko ya sayansi na Teknolojia.

Kwa upande wake Mkufunzi Mkuu wa Chuo Cha Taaluma ya Polisi Dar es salaam DPA kamishna msaidizi wa Polsi ACP Andrew Legembo amesema mafunzo hayo yatawaongezea uwezo wa kimedani maafisa na wakaguzi wasaidizi wanafunzi katika kukabiliana na matishio ya kiusalama katika kutekeleza majuku yao.