Na Mwandishi Maalumu – Dar es Salaam

Wataalamu wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kushirikiana na wenzao kutoka Hospitali ya Jimbo la Shandong la nchini China kuimarisha huduma katika tiba ya upasuaji wa moyo upande wa kupandikiza mishipa ya damu, matibabu ya mishipa ya damu iliyopasuka (dissecting aortic aneurysm), pamoja na matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alipokutana na wajumbe kutoka Serikali ya watu wa China walipotembelea Taasisi hiyo jana kwaajili ya kuangalia huduma zinazotolewa na kujadili maeneo ambayo China itaendelea kushirikiana na JKCI.

Dkt. Kisenge alisema JKCI inaendeleza ushirikiano na Serikali ya Watu wa China ambapo wataalamu mabingwa wabobezi wa magonjwa ya moyo kutoka Hospitali ya Jimbo la Shandong wanatarajiwa kufika JKCI kubadilishana ujuzi na kuifanya JKCI kuendelea kuwa kituo cha ubora Afrika Mashariki na Kati.

“Tumekutana na ujumbe kutoka Hospitali ya Jimbo la Shandong na kukubaliana kuleta madaktari mabingwa waliobobea katika kutoa huduma za matibabu ya moyo ambao wataenda kufanya kazi na JKCI kwa kipindi cha miaka miwili kuongeza ujuzi kwa wataalamu wa JKCI na kutoa huduma kwa wagonjwa wanaohitaji huduma za matibabu ya moyo”, aliesema Dkt. Kisenge.

Dkt. Kisenge alisema kupitia ushirikiano unaoenda kufanyika kati ya JKCI na wataalamu wa afya kutoka Jimbo la Shandong la nchini China kutaenda kuimarisha tiba utalii na kuifanya JKCI kuwa yakibingwa zaidi kwani kwa sasa tayari ni Taasisi ambayo ni kituo cha ubora Afrika Mashariki na kati katika kutoa huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu ya moyo.

“Huko mbeleni tutaendelea kushirikiana na Serikali ya Watu wa China kuimarisha eneo la tiba mtandao (telemedicine) ambapo kwa pamoja tutaweza kumjadili mgonjwa na kumpangia matibabu tukiwa maeneo mawili tofauti kurahishisha matibabu ya wagonjwa wetu”, alisema Dkt. Kisenge

Kwa upande wake mwakilishi kutoka Wizara ya Afya Dkt. Liggyle Vumilia alisema Tanzania na China zimekuwa na ushirikiano wa muda mrefu tangu mwaka 1968 kwa kutuma wataalamu wa afya Tanzania kwaajili ya kubadilishana ujuzi ambapo hadi sasa wataalamu wa afya 11 kutoka nchini China wameshafanya kazi JKCI.

Dkt. Vumilia aliiomba Serikali ya Watu wa China katika kubadilishana ujuzi iangalie namna ya kuwachukuwa wataalamu wa afya wa JKCI na kuwapeleka nchini China ili wakaone namna wenzao wanavyotoa huduma kwani itawasaidia kubadili mifumo waliyojiwekea na kuwa bora zaidi.

“Mkiwekeza katika Taasisi hii mmewekeza katika nchi nyingi za Afrika kwani sasa nchi nyingi za Afrika zinaitegemea JKCI katika kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo”, alisema Dkt. Vumilia

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Tiba kutoka Hospitali ya Jimbo la Shandong Dkt. Mali Xin alisema Serikali ya Watu wa China imekuwa ikidhamiria kutoa huduma bora na msaada kwa wagonjwa wa moyo waliopo Tanzania kwa kutoa wataalamu wa afya mabingwa waliobobea katika magonjwa ya moyo.

Dkt. Mali Xin alisema ushirikiano uliowekezwa kati ya Tanzania na China umeiwezesha JKCI kufanya upasuaji wa moyo wa aina mbalimbali na kupunguza wagonjwa wanaoenda nje ya nchi kwaajili ya kutafuta matibabu.

“Kundi la 27 la wataalamu wa afya kutoka nchini China wakiwemo wataalamu wa magonjwa ya moyo wanatarajiwa kufika nchini Tanzania karibuni, naamini kupitia kundi la wataalamu hao watakaofika hapa JKCI litaenda kuwapa ujuzi mpya wa namna ya kufanya upasuaji wa moyo mbalimbali”, alisema Dkt. Mali Xin.

AM

Alex Sonna 5 hours ago

Share

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza na wageni kutoka Hospitali ya Jimbo la Shandong iliyopo nchini China walipotembelea JKCI jana kwaajili ya kuangalia huduma zinazotolewa na kujadiliana maeneo ya kushirikiana.

Mkurugenzi wa Idara ya Tiba kutoka Hospitali ya Jimbo la Shandong Dkt. Mali Xin akielezea namna ambavyo China imejipanga kushirikiana na JKCI kutoa huduma za kibingwa wakati wajumbe kutoka Hospitali ya Jimbo la Shandong iliyopo nchini China walipotembelea JKCI jana na kukutana na uongozi wa Taasisi hiyo.

Baadhi ya wajumbe kutoka Hospitali ya Jimbo la Shandong iliyopo nchini China wakisikiliza wakati wa kikao na viongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kujadili maeneo ya kushirikiana katika kuboresha huduma za matibabu ya moyo nchini jana katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya wajumbe kutoka Hospitali ya Jimbo la Shandong iliyopo nchini China wakitembelea maeneo ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) walipotembelea Taasisi hiyo jana kwa ajili ya kuangalia maeneo ya kushirikiana.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe kutoka Hospitali ya Jimbo la Shandong iliyopo nchini China na viongozi kutoka Wizara ya Afya walipotembelea Taasisi hiyo jana kwaajili ya kuangalia maeneo ya kushirikiana kuboresha huduma za matibabu ya moyo nchini.