Na Wilson Malima, JAMHURI MEDIA

Mfumuko wa bei za bidhaa na huduma chini Tanzania umepungua hadi kufikia asilimia 4.8 kwa mwaka ulioishia Februari 2023 tofauti na ilivyokuwa asilimia 4.9 kwa mwaka ulioshia Januari 2023.

Mfumuko wa bei wa taifa hupima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi nchini.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) leo Machi 8, 2023, kushuka kwa mfumuko wa bei, inamaanisha kuwa kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia Februari, 2023 imepungua kidogo ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia Januari, 2023.

“Kupungua kwa mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia mwezi Februari, 2023 kumechangiwa na kupungua kwa mfumuko wa bei kwa baadhi ya bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula kwa kipindi cha mwaka ulioishia mwezi Februari, 2023 ikilinganishwa na kipindi cha mwaka ulioishia mwezi Januari, 2023.” Imesema taarifa ya NBS

Kwa upande wa bei za biidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia Februari, 2023 umepungua hadi asilimia 9.6 kutoka asilimia 9.9 kwa mwaka ulioishia Januari, 2023.

“Mfumuko wa bei ambao haujumuishi bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Februari, 2023 umepungua pia hadi asilimia 2.8 kutoka asilimia 3.0 kwa mwaka ulioishia mwezi JanuariI, 2023.” Imesema taarifa ya NBS

Taarifa hiyo imeeleza baadhi ya bidhaa za vyakula zilizoonesha kupungua  kwa mfumuko wa bei kwa mwaka ulioshia Februari, 2023 ikilinganishwa na mwaka ulioshia Januari 2023 kuwa ni pamoja na, ngano (kutoka asilimia 7.7 hadi asilimia 7.1) dagaa wakavu (kutoka asilimia 5.7 hadi asilimia 1.1) na vinywaji baridi (kutoka asilimia 14.0 hadi asilimia 12.7).

Kwa upande mwingine, baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula zilizoonesha kupungua kwa mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia Februari, 2023 ikilinganishwa na mwaka ulioishia Januari, 2023 ni pamoja na bidhaa kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa nyumba (kutoka asilimia 7.9 hadi asilimia 5.0), gesi (kutoka asilimia 9.7 hadi asilimia 9.1), mafuta ya taa (kutoka asilimia 36.9 hadi asilimia 33.1),dizeli (kutoka asilimia 33.1 hadi asilimia 27.8) na bidhaa na huduma kwa ajili ya usafi binafsi (kutoka asilimia 4.2 hadi asilimia 3.7).

Aidha taarifa hiyo imeainisha hali ya mfumuko wa bei kwa baadhi ya nchi za Afrika Mashariki kwa mwaka ulioshia Februari 2023 Kenya ikionyesha kuongezeka kwa mfumko wa bei hadi asilimia 9.2 kutoka 9.0

“Nchini Uganda, mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Februari 2023 umepungua hadi asilimia 9.2 kutoka asilimia 10.4 kwa mwaka ulioishia mwezi Januari, 2023. Kwa upande wa Kenya, mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Februari, 2023 umeongezeka hadi asilimia 9.2 kutoka asilimia 9.0 kwa mwaka ulioishia mwezi Januari, 2023.” Imesema

By Jamhuri