Na Daniel Limbe,JamhuriMedia,Chato

Kanisa Katoliki Jimbo la Rulenge, Ngara, limesema kuwa hata watu wema hufariki dunia.

Kauli hiyo imetolewa leo na Askofu wa Rulenge Ngara, Severine Niwemugizi, wakati akiongoza ibada ya kumwombea toba aliyekuwa Rais wa Tanzania, Dkt. John Magufuli, iliyoambatana na kumbukizi ya miaka miwili ya kifo chake na kufanyika Parokia ya Mlimani Rubambangwe, Chato na kuhudhuliwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wa chama,wana familia pamoja na wananchi mbalimbali.

Akinukuu aya kutoka katika Biblia Takatifu, Askofu Niwemugizi amesema maandiko ya Mfalme Suleiman yanaweka bayana kuwa siyo wabaya tu wanaokufa, bali hata wema pia hufa, ndiyo maana hata Yesu Kristo alikufa akiwa na umri wa miaka 33 pamoja na kwamba alikuwa mtakatifu.

“Je, Yesu Kristo alikuwa mbaya? Watoto wanazaliwa na kufa, vijana nao hufariki dunia wakingali wadogo tu, nao huwa ni wabaya?” anahoji Askofu Niwemuzigi.

Kauli yake imetafsiriwa kuwa ni majibu kwa kauli iliyowahi kutolewa na Katibu Mkuu wa zamani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuph Makamba.

Akizungumza wakati wa mkutano mkuu wa chama hicho mwaka jana, Mzee Makamba alnukuliwa akiisema: “Watu wazuri hawafi!”

Licha ya kauli hiyo kukosolewa na watu mbalimbali, siku moja baadaye Rais Samia Suluhu Hassan aliwaomba radhi Watanzania alipokuwa akitoa hotuba ya kuhitimisha mkutano huo, akisema Mzee Makamba aliteleza ulimi na kuwa hakuwa na nia mbaya.

Akitoa salam kwa niaba ya familia, Janeth Magufuli, mjane wa Rais Magufuli, amelishukuru Kanisa kwa kuendelea kuungana na familia yake kumwombea mpendwa wao.

Akizungumza kwa niaba ya Rais Samia, Waziri wa Ulinzi, Innocent Bashungwa, amemuelezea Dkt. Magufuli kuwa ni kiongozi atakayekumbukwa na vizazi vingi kutokana na maendeleo makubwa aliyotekeleza enzi za uhai wake.

“Ameacha alama kubwa kwa nchi yetu. Rais Samia amenituma kufikisha salamu hizi kwa familia na kwamba anaendelea kuwakumbuka katika siku hii muhimu,” amesema Bashungwa

By Jamhuri