Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) wamelifungia ghala iliyokua ikihifadhi bidhaa mbalimbali ikiwemo mchele kutokana na ghala hiyo kukosa sifa za kuhifadhia bidhaa hizo.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa kushtukiza kuangalia usalama wa chakula,na uhalali wa uwepo wa ghala hilo huko Mpendae Kaimu Mkurugenzi Idara ya Usalama wa Chakula ZFDA Khadija Ali Sheha, amesema kuwa,ukaguzi umebaini kuwa ghala hilo halijasajiliwa,haliko katika hali ya usafi na haliruhusu hewa kupita hali inayopelekea chakula kinachihifadhiwa hapo kutokua salama.

Amesema kuwa usalama wa chakula ni jukumu la kila mmoja hivyo ameitaka jamii kutoa taarifa mapema mara tu wanapoona hali isiyokuwa ya kawaida katika maghala ya kuhifadhia chakula.

“Kwa pamoja sasa tushirikiane kulinda afya zetu kwa kuyafichua maghala kama haya ambayo yanahatarisha afya za watu na kuitia hasara Serikali” amesema.

Aidha katika ukaguzi huo ZFDA wamebaini Kua mmiliki wa ghala hilo amekua akiziba vifungashio vya asili Kwa baadhi ya bidhaa zilozuiliwa kusafirishwa nje ya Zanzibar ikiwemo mchele aina ya mapembe katika maboksi na vipolo ili kurahisisha usafirishaji jambo ambalo ni kosa kisheria.

Kwa upande wake mmiliki wa ghala hilo Saleh Hassan Khamis amesema kuwa amekua akizifunga tena bidhaa hizo katika mapolo na maboksi ili kuzihifadhi na kuziweka salama wanapokua safarini bila kufahamu kufanya hivyo kama ni kosa kisheria, hivyo saleh ameiomba ZFDA kuwapatia elimu Wafanyabiashara ili kuepuka makosa yasiyotarajiwa.

Nae Sheha wa Shehia ya Mpendae suleiman Ali Makuu amewasihi wafanya Biashara kuwa waaminifu na kuwataka wafuate Sheria zilizowekwa na Serikali ili kuepuka matatizo wakati wanapofanya Biashara zao.

Katika ukaguzi huo mbali na bidhaa nyengine jumla ya polo mia tatu za mchele aina ya mapembe yenye ujazo wa kilo hamsini yamekutikana katika ghala hilo ambalo halijasajiliwa.

By Jamhuri