Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Siha

Serikali imetenga kiasi cha shilingi trilioni 6.7 kwaajili ya kuboresha huduma za afya hii ikiwa ni pamoja na kusomesha wataalamu ndani na nje ya nchi ili wananchi wengi waweze kupata matibabu ya kibingwa ya magonjwa mbalimbali yakiwemo ya moyo.

Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel wakati akiongea na wananchi waliofika katika Hospitali ya Wilaya ya Siha kwaajili ya kupata huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu ya moyo zinazotolewa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa hospitali hiyo.

Mhe. Dkt. Mollel ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Siha alisema katika kambi hiyo kwa muda wa siku tatu wataalamu wameona watu 307 kati yao 37 wamekutwa na matatizo yanayohitaji matibabu ya kibingwa na hivyo kupewa rufaa ya kwenda kutibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete.

“Kama hawa watu waliogundulika kuwa na matatizo wasingeonwa katika kambi hii si ajabu wasingeweza kuishi muda mrefu lakini uwepo wa matibabu haya umewasaidia kugundulika kuwa na mamtatizo ambayo yanahitaji matibabu ya kibingwa na watapata matibabu mapema”, alisema Mhe. Dkt. Mollel.

“Huduma za matibabu zinazopatikana katika upimaji huu zinatolewa bila malipo yoyote yale kwani Serikali imegharamia kila kitu na kutokana na uhitaji kuwa mkubwa JKCI wameongeza siku mbili hivyo basi kambi hii itamalizika siku ya Jumapili, ninawaomba wananchi mjitokeze kwa wingi kuja kupima afya zenu”, alisisistiza Mhe. Dkt. Mollel.

Mhe. Dkt. Mollel alimshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha huduma za afya na hivyo kuwafanya watanzania na ambao siyo watanzania kuwa na uhakika wa kupata matibabu ya kibingwa na ndiyo maana Tanzania inapokea wagonjwa kutoka nchi za jirani ambao wanakuja kutibiwa hapa nchini.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt.Peter Kisenge, Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi wa JKCI Dkt. Delilah Kimambo alisema Taasisi hiyo imekuwa ikitoa huduma ya tiba mkoba ijulikanayo kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services ya kuwafuata wananchi mahali walipo na kutoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo.

Pia katika tiba mkoba wanatoa nafasi kwa wale wanaokutwa na matatizo ya moyo kupata nafasi ya kutibiwa mapema kwa kupewa rufaa na kuwajengea uwezo wataalamu wa hospitali husika ili baada ya kumalizika kwa kambi ya matibabu nao waweze kuwatambua na kuwatibu wagonjwa wa moyo.

Dkt. Delilah ambaye pia ni daktari bingwa wa moyo alisema kwa muda wa siku tatu tangu kuanza kwa kambi hiyo ya matibabu wameona watu 307 na kuna ambao wamekutwa na matatizo ya shinikizo la juu la damu. Valvu, mishipa ya damu ya moyo kuziba na kwa upande wa watoto walikutwa na matundu kwenye moyo.

“Siku ya Jumapili tutakuwepo katika mbio za Siha Marathon kwaajili ya kufanya upimaji ninawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kushiriki katika mbio hizi licha ya kushiriki mbio pia mpime afya zenu, mkimbie kwa afya na mlinde mioyo yenu”, alisisitiza Dkt. Delilah.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa wilaya ya Siha Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo Mhe. Duncan Urassa aliishukuru Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kufika wilayani humo na kutoa huduma kwa wananchi.

“Watu wengi wamejitokeza kupima afya zao zoezi hili linatija kwani wananchi wamepewa elimu ya lishe bora ambayo itawasaidia kupambana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwemo ya moyo pamoja na kubadilisha mtindo wao wa maisha”.

“Kuna ambao hawakuwa wanajijua kuwa na magonjwa ya moyo baada ya upimaji wamegundulika kuwa wagonjwa, ninaamini baada ya zoezi hili watu watabadili mtindo wa maisha na kujenga tabia ya kupima afya zao mara kwa mara pamoja na kufanya mazoezi”, alisema Mhe. Urassa.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilala ya Siha Dkt. Haji Mnasi aliwashukuru wataalamu wa JKCI kwa kuwajengea uwezo wataalamu wa Hospitali ya Wilaya ya Siha wa jinsi ya kufanya vipimo vya moyo na  kuwatambua wagonjwa wa moyo jambo ambalo litasababisha wagonjwa wa aina hiyo kutambuliwa na kupata  matibabu kwa wakati.

“Leo hii pia tumekabidhiwa gari na vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 900 ninaishukuru Serikali kwa kujali afya za wananchi wa Siha kwa niaba ya watumishi wenzangu ninaahidi kuvitunza vifaa hivi ili viweze kutumika muda mrefu zaidi” alishukuru Dkt. Mnasi.

Uzinduzi huo ulikwenda sambamba na makabidhiano ya gari moja kati ya matatu yaliyotolewa na Serikali kwa wilaya hiyo ambalo litatumika katika huduma za afya na vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 900 ambavyo vitatumika katika Hospitali ya wilaya ya Siha.

Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Godwin Mollel akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali mara baada ya kumalizika kwa uzinduzi wa kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya moyo inayofanyika katika Hospitali ya Wilaya ya Siha. Kambi hiyo inafanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa wilaya ya Siha.

Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikweye (JKCI) Dkt. Delilah Kimambo akitoa elimu ya matumizi sahihi ya dawa za shinikizo la juu la damu kwa mwananchi aliyefika katika Hospitali ya wilaya ya Siha kwaajili ya kupata huduma za upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo zinazotolewa katika kambi maalumu ya matibabu inayofanyika katika Hospitali hiyo.

Naibu Waziri wa Afya na Mbunge wa jimbo la Siha Mhe. Dkt. Godwin Mollel akizungumza na wananchi waliofika katika Hospitali ya Wilaya ya Siha kwaajili ya kupata huduma za upimaji na matibabu ya moyo zinazotolewa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali hiyo.

Naibu Waziri wa Afya na Mbunge wa jimbo la Siha Mhe. Dkt. Godwin Mollel akizungumza na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wananchi waliofika katika Hospitali ya Wilaya ya Siha kwaajili ya kupata huduma za upimaji na matibabu ya moyo zinazotolewa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali hiyo.

Naibu Waziri wa Afya na Mbunge wa jimbo la Siha Mhe. Dkt. Godwin Mollel akimkabidhi  Mkuu wa Wilaya ya Siha Mhe. Dkt. Christopher Timbuka funguo za gari moja kati ya matatu yaliyotolewa na Serikali kwa wilaya hiyo ambalo litatumika katika huduma za afya. Licha ya kukabidhi gari hilo Mhe. Dkt. Mollel alifungua kambi maalumu ya matibabu ya moyo inayofanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa hospitali ya wilaya ya Siha

By Jamhuri