Serikali imetoa maagizo matatu kwa Wizara ya Maliasili na Utalii na TANAPA katika kukabiliana na changamoto ya moto kwenye maeneo ya hifadhi ikiwemo mlima Kilimanjaro wakati inapojitokeza.

Agizo hilo limetolewa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo bungeni Novemba 3,2022 bungeni jijini Dodoma wakati akitoa ufafanuzi kuhusu kuzuka kwa moto katika hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro.

“Hakikisheni mnaunda kitengo ndani ya TANAPA cha kukabiliana na majanga au maafa yanayotokea ndani ya hifadhi. Pia wekezeni kwenye matumizi ya teknolojia ya kisasa hususan katika tahadhari, utambuzi na uzimaji moto pamoja na kuimarisha shughuli za doria na uokoaji kwa kushirikisha jamii na wadau.’’ amesema.

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuboresha uwezo wa kupambana na majanga kwa kuimarisha sheria za mifumo ya kitaasisi na kutoa mafunzo ya pamoja miongozi mwa vyombo ndani na nje ya nchi. Pia wakati wote itahakikisha upatikanaji wa vifaa vya tahadhari, uokozi na kutoa huduma mapema kwa waathirika.

Majaliwa ametumia fursa hiyo kutoa shukrani kwa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mkoa wa Kilimanjaro, Majeshi, TANAPA, taasisi nyingine za Serikali pamoja na zisizo za Serikali, wananchi wa vijiji vya jirani na hifadhi pamoja na wadau wote walioshiriki kikamilifu katika uzimaji wa moto.

By Jamhuri