Msaka majangili ateswa

Siku 12 baada ya kumwandikia barua nzito, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Peter Mtani, amekamatwa na kuteswa kwa siku saba mfululizo kabla ya kuachiwa wiki iliyopita bila masharti.

Mtani  amekuwa afisa wanyamapori daraja la pili, kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru kuanzia Julai 2008 hadi Novemba 2016.

Katika barua yake aliyomwandikia, Dk Lauren Ndumbaro, ambayo JAMHURI imeona nakala yake, amesema alimwandikia Katibu Mkuu huyo kumweleza hujuma zinazofanywa katika kitengo cha wanyamapori katika wilaya hiyo.

“Katika utumishi wangu kama afisa wanyamapori wilayani Tunduru, nimepata mafanikio ya kukamata pembe za tembo zenye uzito wa kilogramu 560, ikiwa ni pamoja na kufanikisha kukamatwa kwa gari la abiria likiwa na pembe za tembo kilogramu 180.75, gari hilo lilikuwa likitoka Masasi,” inasomeka sehemu ya barua hiyo.

Amesema kutokana na utendaji huo, ofisi hiyo ya wanyamapori imekumbwa na changamoto kadhaa kutoka ndani na nje, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha anaondolewa katika nafasi yake ili kudhoofisha mapambano dhidi ya ujangili.

“Novemba 2016, nilipewa barua ya uhamisho kutoka Idara ya Wanyamapori kwenda Idara ya Elimu ya Sekondari, uhamisho ambao kimsingi unakinzana na kwenda kinyume na ajira yangu kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru,” amesema Mtani.

Akizungumza na JAMHURI, Mtani amesema alikamatwa na Jeshi la Polisi Desemba 21, 2016 na akaachiwa huru siku saba baadaye, huku akiwa ameteswa kwa kupigwa.

“Kuna mtu amejitokeza hapa Tunduru, nahisi anaweza kuwa jangili wa pembe za tembo ama ni mwanasiasa ambaye maslahi yake yametetereka kutokana na jitihada zangu za kupiga vita ujangili ama watumishi serikalini ambao si waaminifu…mtu huyo anasema nashirikiana naye katika biashara hiyo haramu.

“Mtu huyo amediriki kupeleka taarifa Wizara ya Maliasili na Utalii akidai mimi ni mshirika wake wa ujangili, lakini cha kushangaza ni kwamba hadi sasa Polisi na Naibu Waziri wa Maliasili hawajawahi kumuona huyo mtu na wanasema namba yake ya simu haipatikani tangu Polisi waliponikamata na kunitesa,” anasema Mtani.

Mtani anasema kwamba anashangazwa na hatua ya Jeshi la Polisi kumtaka amtaje mshirika wake huyo na mahali alipo ilhali Polisi ndiyo waliowasiliana na mtu huyo kabla hata ya yeye kukamatwa.

“Nilikamatwa kwa shinikizo la Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani, ambaye pia alitoa amri niteswe hadi nimtaje mtu huyo ambaye sijawahi kumuona na wala hata jina lake silijui…nimeteswa sana na Polisi kwa siku nane nikiwa nimevuliwa nguo, nimefungwa pingu na kuning’inizwa kwenye mti huku nikipigwa virungu,” Mtani ameiambia JAMHURI.

Mtani anasema kuwa hatua yake ya kujitoa kupambana na ujangili kwa nafasi yake, huenda kumekwaza maslahi ya watu fulani ndani na nje ya Serikali ambao sasa wamefikia hatua ya kutaka kumpoteza kabisa.

“Mimi kama Mtanzania mzalendo nimeamua kupambana na ujangili kwa nafasi yangu, na hadi sasa nimewezesha kukamatwa kwa kilo 560 za pembe za tembo, jambo hili limewakwaza majangili,” anasema Mtani.

Mtani anasema kuwa kwa upande wake anaona ni bora zaidi kushirikiana na mashirika ya kupambana na ujangili ya kimataifa kuliko kushirikiana na Wizara ama Jeshi la Polisi, maana vyombo hivyo vimekuwa vikichukua uamuzi kabla ya kujiridhisha na jambo husika.

“Mimi msimamo wangu mpaka leo ni kwamba Polisi na Wizara walete FBI, CIA hata mashirika mengine ya kupambana na ujangili, nipo tayari kushirikiana nayo katika vita hii bila hivyo siwezi kwa mateso niliyoyapata,” anasema Mtani.

Mmoja wa maafisa kutoka Wilaya ya Tunduru, ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini, ameiambia JAMHURI kuwa anamfahamu Mtani kama mmoja wa wafanyakazi wenzake ambao wamekuwa wakichapa kazi, lakini katika utendaji wake amegusa maslahi ya baadhi ya madiwani ambao nao wakapeleka mashtaka kwa mbunge, ambaye pia ni Naibu Waziri, Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani.

Mtoa taarifa huyo amesema kumekuwa na vuguvugu la madiwani kutaka kumuondoa kazini, na tayari wamefanikiwa kwa kiwango kikubwa.

“Huyo kijana amekuwa anafanya kazi nzuri, tulisikia amekamatwa bila hata kumhusisha mwajiri wake, walikuja watu kutoka Dar es Salaam…tumeambiwa ameteswa sana na ameachiwa,” kimesema chanzo chetu

Akizungumza na JAMHURI, Naibu Waziri Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani, amesema hajawahi kufanya mawasiliano yoyote kuhusu tuhuma zinazomkabili, huku akisisitiza kwamba kama kuna ushahidi basi utolewe uthibitishe tuhuma hizo.

“Sijui chanzo chako cha hiyo habari kimetoa wapi taarifa hiyo, lakini mimi sijawahi kuandikiwa wala kupewa taarifa yoyote inayomhusu Peter Chrispine Mtani…sijawahi kutoa maelekezo yoyote wala. Kama anasema nimetoa maelekezo hayo awapatie ushahidi kama kweli nahusika na athibitishe kama kweli nimehusika.

“Mtu akiamka tu akatuhumu huo ndiyo unakuwa ukweli? Suala la mtu kukurupuka na kusema najua hapa huyu ni fulani tu, hapa kuna mambo ya kisiasa…mimi sijui chohote kuhusu tuhuma zake za ujangili,” amesema Mhandisi Makani.