Na Mwandishi Wetu,Jamhurimedia,Dar

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla ameelekeza operesheni ya kukamata Mifuko ya plastiki iliyokatazwa kuanza rasmi Jumatatu ya August 29 kwenye Masoko yote ya Mkoa huo.

RC Makalla ametoa maelekezo hayo wakati wa kikao kazi na viongozi wa Masoko yote ya Mkoa huo, Machinga na Maafisa Masoko ambapo pia ameelekeza msako wa kukamata Viwanda Bubu vinavyozalisha Mifuko hiyo kuanza Mara moja.

Aidha RC Makalla ameelekeza kila Wilaya kupitia Kamati za Ulinzi na usalama kuendesha Operesheni hiyo ambapo pia amewataka Maafisa Masoko kwa kila soko kutoa taarifa ya mwenendo wa zoezi Hilo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri husika kila siku.

Tayari RC Makalla amepata baraka zote za Operesheni hiyo kutoka kwa Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango ambae ameelekeza kila Mkoa kufanya Operesheni ya kutokomeza na kuzuia uingiaji wa Mifuko hiyo.

Pamoja na hayo RC Makalla ameelekeza Mamlaka za Udhibiti ikiwemo Baraza la usimamizi wa Mazingira NEMC na TBS kutoa tamko la maelekezo ya usimamizi kwa kila Mkoa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha Elimu inaendelea kutolewa.

Itakumbukwa kuwa mnamo Juni Mosi,2019 Serikali ilitangaza marufuku ya Matumizi ya Mifuko ya plastiki na kufanikiwa lakini hivi karibuni Mifuko hiyo imeanza kurudi kwa Kasi jambo lililopelekea Serikali kutangaza Operesheni ya kutokomeza.

By Jamhuri